Na Albano Midelo,Songea
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema utakapokamilika mradi wa ujenzi wa barabara ya lami nzito kutoka Likuyufusi hadi Mkenda mpakani mwa Tanzania na Msumbiji itakuwa ni fursa kwa wananchi wa Msumbiji kuutumia uwanja wa ndege Songea hivyo kuongeza uchumi wa Mkoa na Taifa.
Kanali Abbas amesema hayo wakati anazungumza katika Kituo cha Uhamiaji cha Mkenda wilayani Songea baada ya kukagua miundombinu ya barabara hiyo yenye urefu wa Zaidi ya kilometa 120.
Amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutenga Zaidi ya shilingi bilioni 74 kuanza kutekeleza awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara ya lami kilometa Zaidi ya 60 kuanzia Likuyufusi hadi njia panda ya Muhukuru wilayani Songea.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuamua kuunganisha Mkoa wa Ruvuma na nchi ya Msumbiji kwa kuanza kujenga barabara ya lami kilometa 60 ’’,alisema RC Abbas.
Mkuu wa Mkoa pia amemshukuru Rais Dkt Samia kwa kutoa fedha za upanuzi na ukarabati wa uwanja wa Ndege Songea ambapo serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 37 kutekeleza mradi huo.
Hata hivyo amesema ujenzi barabara ya Likufusi – Mkenda mpakani na nchi ya Msumbiji,itakuwa fursa kwa wananchi wa nchi hiyo kutumia barabara hiyo hadi mjini Songea kisha kutumia uwanja wa ndege wa Songea kusafiri sehemu mbalimbali nchini.
Amesisitiza kuwa Rais Samia amewaagiza kuzitumia fursa zilizopo mkoani Ruvuma kwa kutoa fursa na kufungua shughuli za kiuchumi katika Mkoa wa Ruvuma bila kuathiri suala zima la ulinzi na usalama katika Mkoa ambao upo mpakani na nchi za Msumbiji na Malawi.