Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara l, Dkt Suleiman Hassan Serera akifungua kikao cha kujadili mradi wa kuboresha upatikanaji wa huduma za maji vijijini kwa ubia na sekta binafsi (PPP) ulioandaliwa na mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA).
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
BAADHI ya wafugaji Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameonywa kutoharibu miundombinu inayosambaza maji kwa jamii, kwa kukata mabomba na kunywesha mifugo.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera ameyasema hayo mji mdogo wa Orkesumet kwenye uzinduzi wa mradi wa kuboresha huduma ya maji na usafi wa mazingira vijijini kwa ubia na sekta binafsi (PPP).
Amesema siyo vyema baadhi ya wafugaji kuhujumu miundombinu ya maji kwa kukata mabomba kwa sime ili kuwapa mifugo maji kwenye maeneo yasiyo rasmi.
“Maji ni uchumi na Serikali imetumia fedha nyingi kuwafikishia maji mahali mlipo hivyo tunzeni miundombinu ili iwe faida kwenu na kizazi kijacho,” amesema Dk Serera.
Amesema ameshatoa maelekezo kwa vyombo vya ulinzi na usalama kushirikiana na jamii kuwabaini wahusika ili wachukuliwa hatua.
Meneja wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilayani Simanjiro mhandisi Joanes Martin amesema mradi huo utaboresha upatikanaji wa huduma ya maji.
Mhandisi Martin amesema upatikanaji maji Simanjiro ni asilimia 66.7 na mradi huo utakuwa wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi.
Ofisa wa RUWASA makao makuu Emmanuel Burton amesema mradi huo utanufaisha mikoa mitano ya Manyara, Lindi, Migogoro, Dodoma na Kagera na wilaya 15.
Burton amesema kwenye mkoa wa Manyara, wilaya zitakazonufaika na mradi huo ni Simanjiro, Kiteto na Mbulu.
Katibu wa CCM wilaya ya Simanjiro, Amos Shimba amempongeza meneja wa Ruwasa Simanjiro mhandisi Joanes Martin kwa namna anavyosimamia sekta ya maji kwa uhakika.
“RUWASA Simanjiro inatekeleza ilani ya uchaguzi wa CCM ya kuhakikisha jamii inapata maji kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025, tunawapongeza sana,” amesema Shimba.
Mmoja kati ya wafugaji wa kata ya Langai, Elias Merika amesema baadhi ya wanaoharibu miundombinu kwa ajili ya kuwapa mifugo wanafanya makosa makubwa.
“Wanapaswa kutambua kuwa serikali imetumia gharama kubwa hivyo hawapaswi kufanya uhalifu na watatoa ushirikiano kuwabaini wahusika wakamatwe,” amesema.