MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mary Chatanda, akizungumza leo Machi 25,2024 jijini Dodoma kwenye semina ya usambazaji na mafunzo ya matumizi ya matokeo ya sensa kwa viongozi wa kisiasa kanda ya kati
…………..
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mary Chatanda amesema kuwa anakerwa na baadhi ya wanaharakati wanaotoka mitandaoni na kuanza kusema hawajaona kilichofanywa na Rais Samia kwa madai ya katiba,
Akizungumza leo Machi 25,2024 jijini Dodoma kwenye semina ya usambazaji na mafunzo ya matumizi ya matokeo ya sensa kwa viongozi wa kisiasa kanda ya kati amesema kuwa wao kama UWT hawatokaa kimya kuyatangaza mafanikio yaliyoletwa na Rais Samia.
“Kuna wanaharakati akiwemo Dokta Ananilea Nkya amekuwa akimzungumzia Rais DK.Samia kuwa hakuna alichokifanya katika uongozi wake , hebu atoke akajionee mambo aliyoyafanya Rais na siyo kuongea huku akiwa amekaa”amesema.
Amesema Rais Dk,Samia atapimwa kwa namna anavyotekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 ambapo katika kipindi cha miaka mitatu ameitekeleza kwa kishindo na kiwango cha juu tangu nchi ipate uhuru.
“Wanaharakati wasiturudishe nyuma wengi tunaimani na Rais Dk.Samia na tunamuunga mkono kwani ameonyesha uwezo mkubwa ndani na nje ya nchi na amepata tuzo,”alisema
Amesema Rais ameleta mafanikio mengi ikiwemo ukamilishaji wa ujenzi wa Ikulu ya Dodoma,ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, Daraja la Busisi Mwanza ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 80 na Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Pamoja na hayo amesema kuwa Demokrasia imeimarishwa kuliko kipindi chochote tangu kuanzishwa kwa vyama vingi, “vyama vinafanya mikutano ya hadhara na kuandamana tena kwa kupewa ulinzi wa kutosha, uhuru mkubwa wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kutumia mitandao mpaka unapitiliza.
Wakati huohuo Mwenyekiti huyo amewataka viongozi hao kuyafanyia kazi mafunzo wanayopewa kwani nimuhimu sana hasa katika kipindi cha uchaguzi
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa UWT Jokate Mwegelo, amesema semina hiyo ni muhimu kwasababu itahamasisha wanawake kujitokeza katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
“Semina hii ni muhimu kwasababu itaenda kufungua milango kwa wanawake kujitokeza kwa wingi katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla,”amesema.
Awali akizungumza katika mafunzo hayo Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Tanzania Bara, Spika Mstaafu Anne Makinda amesema Rais Dk.Samia amefanya mambo makubwa hivyo ni kazi kwa wanawake kuendelea kumuunga mkono.
Amesema katika historia yake ya uongozi hakuwahi kufikiria kama Tanzania itaongozwa na mwanamke hivyo ujio wa Rais Dk.Samia ni baraka kwa Taifa
“Kazi kubwa zimefanyika na serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka mitatu hivyo ni muhimu sisi wanawake tukaendelea kumuunga mkono Rais Dk.Samia ili afanye mambo makubwa zaidi,”amesema.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk.Albina Chuwa amesema Rais Dk.Samia amewezesha kufanyika kwa sensa ya kidigitali zaidi ambapo waliweza kukusanya na takwimu za majengo.
Kaatika awamu hii wameweza kufanya tadfiti mbalimbali ambazo zinaonyesha kuwa Tanzania inaendelea kupiga hatua katika kuboresha huduma kwa wananchi.
“Rais Dk.Samia maefanya mambo makubwa na mazuri kwa upande wa NBS tumefanikiwa kufanya sensa ya kidigitali ambapo nchi nyingine zinakuja kujifunza kwetu na wengine wanaomba wataalamu kutoka kwetu kwa ajili ya kuwasaidia,”amesema