Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), Mheshimiwa Stansalaus Mabula akiwa na wajumbe wa Kamati hiyo wakikagua ujenzi wa msingi katika moja ya wodi ya Hospitali ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Marawakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Hospitali hiyo.
….
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), imeielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuhakikisha inafuata taratibu na sheria zote za manunuzi wakati wanapotekeleza miradi mbalimbali ya Serikali.
Maelekezo hayo yalitolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Stansalaus Mabula wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Mheshimiwa Mabula alisema pomoja na kutozingatia taratibu za manunuzi lakini pia Halmashauri hiyo imeshindwa kujibu hoja 10 za ukaguzi kwa kushindwa kumkabidhi mkaguzi nyaraka alizozihitaji, hivyo Kamati inataka vielelezo vyote vya hoja hizo vipatikane na akabidhiwe mkaguzi.
Alitoa mfano kwamba katika kipindi cha miaka mitatu kila mwaka kiasi cha mapato ya ndani yanayokusanywa yasiyopelekwa benki kimekuwa kikiongezeka kila mwaka.
“Kamati inaagiza taratibu na sheria ndogo za ukusanyaji mapato mlizojiwekea zifuatwe kwa sabababu kwa kwenda kinyume na taratibu hizo ni uvunjifu wa sheria na inawezekana kuna njama za kuiibia Serikali.
“Tunataka kila mapato yanayoingia kwenye Halmashauri yaingizwe kwenye kumbukumbu ili mkaguzi akihitaji nyaraka apatiwe, Kamati inaagiza nyaraka zote alizohitaji mkaguzi apatiwe,” alisema.
Aidha, alimtaka Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri hiyo kuwa jicho la ndani la Halmashauri hiyo ili aweze kumsaidia Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Halmashauri.
“Watumishi wengi hapa ni wapya, mnalo jukumu la kuifanya Serengeti kuwa mpya, msaidieni Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi na wananchi wa Serengeti kwa ujumla,” alisema.
Kuhusiana na ujenzi wa Hospitali Kamati ilitaka majengo ambayo bado hayajakamilika yakamilishwe mapema iwezekanavyo pamoja na kufanya marekebisho katika maeneo ambayo Kamati imeyaainisha.