Nchi Wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC) zimetakiwa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa nchi
zao zinakuwa na amani, Umoja na utulivu na kutafuta ufumbuzi wa migogoro kwa
kutumia njia zao wenyewe.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Mkutano wa
Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC
ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa
Zambia, Mhe. Mulambo Haimbe wakati anafungua Mkutano huo uliofanyika jijini
Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.
Tanzania inatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi
hiyo baada ya Zambia na katika
Mkutano huo, Tanzania
inawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe
January Makamba (Mb) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt.
Stergomena Tax (Mb).
Mkutano huo pamoja na mambo mengine unapokea
ripoti ya utekelezaji wa vikosi vya kulinda amani katika Jimbo la Cabo Delgado
nchini Msumbiji na mchakato unaoendelea wa kupeleka vikosi vya kulinda amani Mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Nchi Wanachama zimehimizwa kuimarisha zaidi mshikamano
na kuchangia rasilimali walizonazo
ili kuviangamiza vikundi vya waasi vinavyotishia amani kwenye Kanda ya SADC.
Imeelezwa kuwa bila ya amani na Usalama katika Kanda hiyo, wananchi wasitarajie
kufikiwa kwa mtangamano na maendeleo ya kweli.
Mkutano huo wa Mawaziri ni maandalizi ya
Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya SADC
utakaofanyika Machi 23, 2024 ambapo Tanzania itawakilishwa na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.
Wajumbe wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika Lusaka, Zambia Machi 22, 2024. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe January Makamba (Mb), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (kulia) wakiimba nyimbo za taifa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika Lusaka, Zambia Machi 22, 2024. |