Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Slaa akizungumza na wananchi wakati akisikiliza kero zao
Wananchi mbalimbali waliojitokeza kuleta kero zao katika viwanja vya Ngarenaro mkoani Arusha .
Happy Lazaro ,Arusha .
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Slaa ameweka kambi mkoani Arusha kwa muda wa wiki moja kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi wa hapo hapo.
Aidha waziri amesema umefika wakati wa kumaliza migogoro ya ardhi iliyodumu kwa miaka zaidi ya thelathini katika mkoa wa Arusha.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kuleta kero mbalimbali zinazohusu Wizara yake katika viwanja vya Ngarenaro Jijini hapa amesema atashirikiana na viongozi wengine wa Mkoa kutatua kero hizo na kuwataka wananchi kuendelea na majukumu yao ya kujiingizia kipato kwani matatizo yanaenda kufika kikomo.
“Nimepokea malalamiko yenu na niwape pole sana kwani mmehangaika kwa miaka mingi bila majibu, lakini sasa itoshe kusema kuwa mwarobaini unaenda kupatikana”amesema Slaa.
Amesema kuwa ,kwa kipindi hiki wanahitaji ushirikiano wa kutosha kutoka kwa Mkuu wa mkoa wa Arusha ,John Mongela ambaye kwa sasa yupo Dodoma katika vikao vya bajeti vinavyoendelea Bungeni na hivyo akirudi kila kitu kitalaa sawa .
Aidha ameongeza kuwa mgogoro mingi ya ardhi ni ya miaka mingi na imekuwa ya kurithishana kizazi hadi kizazi suala linaloharibu taswira ya nchi.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya OldonyoSambu Raymond Lairumbe aliyeziwakilisha kaya 371, amesema ni wakati sasa wa mgogoro wa ardhi yao kuisha kwani ni wa muda mrefu na umetesa watu sana.
Amefafanua kuwa,eneo lao linazidi kuwa dogo kulingana na watu kuongezeka ilihali ardhi yao iliporwa na kumilikiwa na watu wenye nguvu ambao serikali iliwafumbia macho.
“Mimi ni mhanga wa mgogoro wa Kata ya OldonyoSambu, mwaka 1998 wakati wa kupigania kukomboa ardhi yetu nilipigwa na kukatwa katwa mapanga ya kichwa mikono na sehemu zingine za mwili, nilifanywa mlemavu, labda ilikuwa mpango wa Mungu siku moja niwatetee hawa wananchi kupata haki yao, na sasa kwa ujio huu wa Waziri Silaa kama alivyotuhakikishia nina imani haki yetu itapatikana”.ameeleza Diwani huyo.
Wakati huohuo Mama Ngereza mkazi wa kata ya OldonyoSambu anayewakilisha kaya iliyodhulumiwa ardhi amesema suala hilo wasiachiwe viongozi wa wilaya wala Mkoa bali Waziri mwenyewe awapambanie hadi haki ipatikane.
Zoezi la kusikiliza kero za wananchi linaendelea kwa muda wa wiki moja katika viwanja vya Ngarenaro Jijini Arusha,ambapo amewataka wananchi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kueleza kero zao zilizodumu kwa muda mrefu ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.