Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa leo Machi 22, 2024 amaezindua ripoti ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Vijiji Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi na kutoa vyeti 18 vya ardhi ya kijiji.
Waziri Mkuu amefanya uzinduzi huo katika Mkutano wa wadau wa kujadili utekelezaji mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi, uliohusisha wadau wa masuala ya ardhi kutoka maeneo mbalimbali wilayani Ruangwa.
Waziri Mkuu amesema kuwa lengo la Serikali ni kupima ardhi yote nchini ili wananchi wakiwemo wanavijiji ili waweze kuitumia ardhi hiyo kufanya shughuli zao za kiuchumi.
Aidha, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi ambao Halmashaui zao zinanufaika na mradi washirikiane na Wizara ya Ardhi kufanikisha mradi huo.
“Nasisitiza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyeviti na watendaji katika vijiji washiriki kikamilifu kuwafikia wananchi na kuwaelimisha umuhimu wa matumizi sahihi ya ardhi ili waweze kunufaika na kupata hati miliki za ardhi wanayoimiliki” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri mkuu ameongeza kuwa juhuhudi zinazofanyika za kupima ardhi nchini ni matokeo ya utendaji kazi na usimamizi mzuri unaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia suluhu Hassan.
“Mhe. Rais amekuwa mstari wa mbele katika kusisitiza juu ya upimaji wa ardhi, hata nilipomuambia nakuja huku amenipa salam zenu na anafuatilia hiki kinachondelea kupitia vyombo mbalimbali vya habari na serikali yake itatenga bajeti kwa ajili ya kazi ya upimaji” Waziri Mkuu Majaliwa.
Awali akimkaibisha Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda, amesema mradi huo utavifikia vijiji vyote katika wilaya ya Ruangwa, ili kuhakikisha kuwa mpango wa matumizi bora vijijini unapata mafanikio makubwa.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na kasi kubwa ya ukuaji wa miji na vijiji kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu linalosababisha kuongezeka kwa mahitaji ya ardhi iliyopangwa na yenye usimamizi mzuri na salama”.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kukabiliana na changamoto hizo kwa kufanya maboresho mbalimbali ya huduma za Sekta ya Ardhi, kuhuisha miundo ya Wizara na kubuni programu na miradi mabalimbali kama vile programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha na Programu ya Urasimishaji wa Makazi yaliyojengwa kiholela” ameeleza Naibu Waziri Pinda.
Amewataka Madiwani wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano kwa Serikali kupitia maafisa wanaotekeleza mradi huo ili kuwafikia wananchi wao kwa wakati uliopangwa na kuwawezesha kutumia ardhi kwa matumizi sahihi.
“Mradi huu utasaidia sana kupunguza migogoro katika vijiji, kwani utawezesha kila mwanakijiji kufahamu matumizi sahihi ya adhi iliyopo katika eneo lake na kuifahamu mipaka ya eneo lake jambo ambalo litaepusha changamoto nyingi”
Wananchi wa Ruangwa wanafanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwepo kilimo, ufugaji na shughuli za madini ambavyo vyote hivi huwezi kuvitenganisha na matumizi ya ardhi ili kuharakisha shughuli hizo maendeleo.
Akitoa salam za wananchi wa Ruanga kwa Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya hiyo Hassan Ngoma ameishukuru Serikali kwa juhudi inazozifanya katika kushughulikia masuala ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini hali ambayo inaenda kumaliza changamoto zinazowakabili wananchi.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amemshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kuendelea kuwapigania wananchi wa wilaya hiyo kupata miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya ya Ruangwa na wanaunga mkono yale yote yanayoyafanywa kwa ajili ya wananchi wa Ruangwa na Tanzania kwa ujumla.
Mradi wa Uborshaji wa Usalama wa Miliki za Adhi (LTIP) unasimamiwa na Wizara ya Adhi Nyumba na Mandelo ya Makaazi ukiwa na kaulimbiu inayosisitiza usawa wa kijinsia katika kumiliki wa ardhi kwa ustawi wa jamii.