Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mheshimiwa Stansalus Mabula akizungumza jambo wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa Soko hilo katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Stansalus Mabula wakionyeshwa mchoro wa ramani ya Soko Kuu la Kisasa lililopo katika Halmashauri ya Mji wa Tarime wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa Soko hilo.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Stansalus Mabula wakikagua mradi wa ujenzi wa Soko Kuu la Kisasa lililopo katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.
………………
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), imeipongeza Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa matumizi mazuri ya fedha katika ujenzi wa mradi Jengo la Utawala la Halmashauri hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Stansalaus Mabula wakati Kamati alipotembelea mradi huo pamoja na Mradi wa Ujenzi wa Soko la Kisasa katika Halmashauri hiyo.
Alisema Jengo hilo ni zuri ukilinganisha na majengo mengi ambayo Kamati imeshayatembelea na kuyakagua.
“Kamati inatoa pongezi kwa namna mlivyotumia fedha vizuri ambazo zimesaidia kujenga uzio, kibanda cha mlinzi na kukunua baadhi ya samani na bado mmebakiza Shilingi Milioni 82,” alisema.
Aidha, alisema Kamati inaelekeza Halmashauri hiyo kuzingatia taratibu zote katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi kuanzia ngazi ya manunuzi pamoja na kujibu hoja za kiukaguzi zilizojitokeza na kuziwasilisha.
Kuhusiana na mradi wa soko, Mheshimiwa Mabula alisema Kamati inaelekeza mradi ukamilike kwa wakati kwa kuwa muda umeshaongezwa kwa zaidi ya mara nne nje ya mkataba.
“Mjitahidi huu muda wa tarehe 17 Mei, 2024 uwe muda mwisho wa kukamilisha mradi kwa kuwa fedha iliyotumika katika ujenzi wa mradi huu haitakuwa na thamani kama mradi hautakamilika,” alisema.
Alielekeza pia Halmashauri kupanga vizuri bei za vizimba kwa kufanya utafiti vizuri.