Na Paul Mabeja, DODOMA
IKIWA ni miaka mitatu sasa tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani watu wenye ulemavu nchini wamelipongeza Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) kwa namna ambavyo limeweza kutafsiri mwelekeo na maono ya Rais kusaidia kundi hilo kujikwamua kiuchumi kupitia fursa mbalimbali.
Mkurugenzi wa Shirika linalojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu la Foundation For Disabilities Hope (FDH) Maiko Salali alisema kwa muda wa miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia STAMICO, imefanikiwa kuyafikia makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu na kuwaunganisha na fursa mbalimbali.
“Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani mwaka 2021 STAMICO imefanikiwa kuwafikia watu wenye ulemavu na kuwaunganisha na fursa mbalimbali ikiwemo uuzaji wa mkaa mbadala wa Rafiki briquettes”alisema Salali
Aidha, alisema katika kipindi hichi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia jumlya ya watu wenye ulemavu 1,500 wamenufaika na fursa hiyo ya uuzaji na uwakala wa mkaa huo mbadala unaozalishwa za STAMICO, kutokana mabaki ya makaa ya mawe.
“Katika miaka hii mitatu sisi watu wenye ulemavu nchini tumenufaika sana kupitia Shirika hili la STAMICO kwa kupata fursa hii ya kuuza mkaa huu ambao ni rafiki wa mazingira na wengine wamepata uwakala wa bidhaa hii katika mikoa mbalimbali nchini na kujikwamua kiuchumi”alisema
Kadhalika, alisema wanampongeza Rais Samia kwa jitihada zake za kupambana na athari za mabadilko tabia nchi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kuondokana na matumizi ya kuni na makaa yanayochangia uharibifu wa mazingira.