Na Prisca Libaga Arusha
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafirishaji Ardhini (LATRA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa elimu juu ya madhara ya usafirishaji haramu wa dawa za kulevya na kemikali bashirifu kwa madereva bodaboda na bajaji zaidi ya 200 wa Wilaya ya Arusha.
Aidha, madereva hao wa Bajaji na Bodaboda wameahidi watakuwa mabalozi wazuri wa kupinga dawa za kulevya na kufikisha elimu juu ya madhara ya tatizo la dawa za kulevya kwa madereva wenzao na jamii kwa ujumla.
Akiongea wakati akitoa mada katika kikao cha wadau wa usafirishaji kilichofanyika Jijini Arusha Afisa wa Mafunzo na Elimu wa Mamlaka DCEA Shabani Miraji amesema kuwa zoezi hilo ni endelevu kuhakikisha matumizi ya dawa za kulevya nchini yanapigwa vita kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali.
Amesema kwamba wasafirishaji hao ni sehemu muhimu ndio maana wamekuwa wakiwapa Elimu ya mara kwa mara kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya nchini inakuwa historia ambapo wadau hao wakishirikishwa vyema kutoa elimu ya udhibiti na matumizi ya dawa hizo Zoezi hilo litakuwa rahisi kudhibiti usafirishaji na matumizi.
Awali akiongea mara baada ya kikao hicho Afisa udhibiti wa Kemikali bashirifu kanda ya kaskazini Thomas Muhesa ameeleza kwamba wamekutana na kundi Kubwa ambao wanatoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo mbalimbali kutoka sehemu Moja kwenda nyingine.
“Kwanini tunasema ni kundi Kubwa na muhimu kwa Jamii yetu ni kwa sababu kwenye dhana ya upambanaji wa dawa za kulevya wasafirishaji ndio wamekuwa wahanga wakubwa sana kwa maana kwamba wanasafirisha dawa za kulevya kama bangi mirungi na heroin lakini pia wanaweza kusafirisha Kemikali bashirifu ambazo zinatengeneza dawa za kulevya lakini wanaweza kusafirisha dawa tiba zenye asili ya kulevya”.
Alisema kwamba wasafirishaji hao kwa mfano maeneo ya mipaka kama Namanga bidhaa nyingi zinaingia kama dawa tiba zenye asili ya dawa za kulevya zinaingia nchini wapo wanaotumia mianya hiyo kwa kuwatumia wasafirishaji hao kwa kutokuwa na ule uelewa wa kutosha ni nini wanakibeba na nini wanakipeleka mahali gani basi hii ndio Njia ya hao kuweza kusafirisha dawa hizo na Kemikali bashirifu.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Maafisa usafirishaji (bodaboda) Hakim Msemo amesema kwamba kupewa heshima ya ubalozi kwa Maafisa hao wa usafirishaji kutapelekea kuweza kutokomeza dawa hizo kwa sababu dawa za kulevya zimekuwa ni tatizo ndani ya nchi yetu watu wanayauza na vijana wanayatumia na kukosa muelekeo na kuharibu nguvu Kazi ya taifa.