Katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi, Mhe. Phaustine Kasike, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Msumbiji alikutana na Rais wa Chemba ya Biashara ya Msumbiji, Bw Alvaro Massinga tarehe 19 Machi, 2024 kwenye Ofisi za Chemba hiyo zilizopo Jijini Maputo.
Kupitia mkutano wao, Viongozi hao wawili walizungumza masuala mbalimbali ya Ushirikiano katika Sekta ya Biashara na Uwekezaji kwa maslahi ya nchi hizi mbili.
Aidha, kwa kuzingatia uhusiano wa kidugu na wa kihistoria baina ya Tanzania na Msumbiji, Viongozi hao walikubaliana juu ya umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uchumi na kuzishauri Taasisi zinazohusika na Masuala ya Uchumi, Biashara na Uwekezaji kufanya kazi kwa ukaribu ikiwemo kushiriki katika Maonesho na Matukio mengine muhimu ya Kiuchumi yanayofanyika katika nchi hizi kila mwaka ikiwemo Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba (Tanzania) na Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Maputo – FACIM (Msumbiji).
Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania – Maputo
19 Machi, 2024