Na Lucas Raphael,Tabora
Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Tabora (WETCU 2018 LTD) kimepitisha mapendekezo ya bajeti ya shilingi bililion 5.07 kwa ajili ya utekelezaji shughuli za Ushirika kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Bajeti hiyo iliwasilishwa na Meneja Mkuu wa WETCU Samwel Jokeya kwenye Mkutano Mkuu wa Chama hicho uliofanyika juzi na jana katika ukumbi wa shule ya sekondari Themi Hill iliyopo katika kata ya Ipuli Mjini Tabora.
Alisema kuwa Chama hicho kinatarajia kupata kiasi cha sh bil 5.07 ambapo kiasi cha sh bil 3.299 zitatokana na ushuru wa mauzo ya zao hilo na kiasi cha sh bil 1.08 kitatokana na gawio la faida ya hisa za benki ya CRDB.
Aidha alibainisha kuwa kiasi cha sh mil 8 kinatarajiwa kupatikana kutokana na gawio la hisa za benki ya Exim na kiasi cha sh mil 653.24 kitatoka kwenye vyanzo vingine vya mapato ya Ushirika (Union).
Jokeya alifafanua kuwa kutokana na mwenendo wa kilimo cha zao hilo Mkoani hapa hususani kwa Wilaya za Tabora, Sikonge, Uyui na Nzega, Union ina malengo ya kuzalisha vyama wanachama ambavyo vinapata pembejeo zao wenyewe.
Hivyo wanategemea kupata ushuru wa takribani sh bil 3.324 kutokana na kilo mil 44.8 zinazokisiwa kuzalishwa na kuuzwa katika msimu wa kilimo wa 2024/2025 kwa kiwango cha ushuru wa Dola 0.03 kwa kila kilo ya tumbaku sawa na sh 73.65.
Alifafanua mapato mengine kuwa ni sh mil 50.2 zinazotarajiwa kukusanywa kutoka kwenye pango la nyumba za Union, upangishaji kiwanja, maghala yaliyopo maeneo mbalimbali katika halmashauri ya manispaa Tabora na ofisi.
Vyanzo vingine ni malipo ya II ya mizani (digital scale) iliyonunuliwa mwaka wa fedha 2021/2022 ya sh mil 33.5, mauzo ya mizani (digital scale) ya sh mil 22.9 ambayo ni asilimia 50 ya thamani ya mizani, aidha wanatarajia kupata sh mil 580 kutokana na tengo la gharama za usimamizi wa pembejeo.
Meneja Mkuu alibainisha kuwa wanatarajia kutumia kiasi cha sh bil 3.304 kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo kuhudumia wakulima ambapo wanatarajia kutumia sh mil 541.34.
Nyingine ni gharama za utumishi ambapo wanatarajia kutumia kiasi cha sh mil 582.97, gharama za uendeshaji (utawala) sh bil 1.72, gharama za kibiashara sh mil 404.09, gharama za kibenki sh mil 17 na matumizi ya dharura sh mil 30.