Na Mwandishi wetu, Babati
MKUU wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ameziagiza Halmashauri za wilaya za mkoa huo kuhakikisha zinafuatilia madeni ya watu waliochukua mikopo ya asilimia 10 na kuzirejesha.
Amewataka wakuu wa wilaya kushirikiana na viongozi hao kufuatilia madeni hayo ikiwemo kuwakamata na kuwakeka ndani wale wasiorejesha mikopo yao.
Sendiga akizungumza mjini Babati kwenye kikao cha ushauri cha mkoa huo (RCC) amesema viongozi hao wanapaswa kufuatilia ipasavyo mikopo hiyo ili irejeshwe.
Amesema hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo la kurejeshwa kwa mikopo hiyo ya mapato ya ndani ya asilimia 10 ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu hivyo nao wanapaswa kusimamia hilo.
“Tunapaswa kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa ili serikali inapojipanga upya itukute sisi Manyara nasi tumeshajiandaa kwa watu wetu kurudishwa mikopo waliyoikopa,” alisema Sendiga.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema waliochukua mikopo hiyo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanapaswa kurejesha.
“Kwa upande wetu viongozi kila mmoja anapaswa kuhakikisha anasimamia hili ili mikopo hiyo irejeshwe kwa wale wote waliokopa kwani wanajulikana kwa kila halmashauri,” amesema Ole Sendeka.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hanang’ Rose Kamili amesema baadhi ya madiwani wameshiriki kuchukuliwa kwa mikopo hiyo hivyo wanapaswa kuhakikisha inarejeshwa.
“Baadhi ya madiwani wa viti maalum wamepitia mlango wa nyuma kwa kutumia wanawake na kuchukua na baadhi ya madiwani wa kata wamewatumia wake zao kukopa hivyo wanapaswa kubanwa ili irejeshwe,” amesema Kamili.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amesema kwa upande wao, wanaiunga mkono serikali katika kurejeshwa kwa mikopo hiyo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani.
“Tupo pamoja na serikali katika hili, nasi Simanjiro tunawataka wote waliochukua mikopo hiyo wairejeshe kwani ilikuwa na muda wa kikomo na sasa umefika waliokopa wanapaswa wairejeshe,” amesema Kanunga.