NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju ,akizungumza leo Machi 18,2024 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha uwasilishaji wa viashiria vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa mwaka 2030.
Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi.Subisya Kabuje,akizungumza wakati wa kikao kazi cha uwasilishaji wa viashiria vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa mwaka 2030.
Mwakilishi wa shirika la kuhudumia watoto Duniani (UNICEF) Mlemba Abassy,akizungumza wakati wa kikao kazi cha uwasilishaji wa viashiria vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa mwaka 2030.
BAADHI ya washiriki wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju (hayupo pichani) ,wakati wa kikao kazi cha uwasilishaji wa viashiria vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa mwaka 2030.
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju ,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua kikao kazi cha uwasilishaji wa viashiria vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa mwaka 2030.
Na.Erick Mungele-DODOMA
SERIKALI imesema suala la malezi na makuzi ni mtambuka hivyo kila mtu anao wajibu wa kuhakikisha taifa linakuwa na kizazi ambacho kitakuwa kinajitambua ili kuweza kusimamia rasilimali zao.
Hayo yamesemwa leo Machi 18,2024 jijini Dodoma na Naibu Katibu mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju wakati wa kikao kazi cha uwasilishaji wa viashiria vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa mwaka 2030.
Mpanju amesema kuwa eneo la makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto ni eneo nyeti sana kwa taifa letu leo hii tunaweza tukawa tunawekeza katika vitu kama ardhi, barabara lakini kama tutakuwa taifa ambalo halina watu ambao wako timamu kichwani itakuwa shida.
“Kama utafiti unavyo onyesha kuwa asilimia 53 ya watoto wapo katika hatari ya kutofikia ukuaji timilifu hali hii ni mbaya sana kwa taifa kwani hatuwezi kuwa na viongozi wa badaye, lakini pia migogoro itakuwepo mingi kwakuwa tuu na rasilimali watu ambayo haijapa malezi na makuzi timilifu”amesema Wakili Mpanju
Aidha, amezitaka halmashauri zote nchini kutenga bajeti ambazo zitasaidia kuwezesha malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika maeneo yao.
Amewataka Wazazi, walezi, jamii na serikali kuweka mifumo ya kuwafatilia watoto waweze kulelewa sawasawa na sayansi ya malezi na makuzi pia kuzingatia lishe inayotakiwa katika malezi sahihi yanayo shahuriwa kiustawi, kisaikolojia kiafya, uchangamfu na menigine yote ikiwa kupata tiba zote sahihi kwa wakati.
“Kama hatutachukua hatua tunaweza kuwakosa Marais wa badaye, Madaktari lakini pia raia wema ambao watakuwa tayari kulitumikia taifa lao na kulinda rasilimali zilizopo nchini.
“Pia tunaweza kuwa na kizazi cha ajabu ambacho hata hakina uwezo wa kusimamia rasimali zao kama hatuta wekeza kwenye malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto”amesisitiza
Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi huduma za ustawi wa jamii, ofisi ya Rais TAMISEMI Bi.Subisya Kabuje amesema serikali inaendelea kutekeleza programu jumuishi ya Taifa ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya Mtoto katika kuhakikisha watoto wote nchini wanafikia ukuaji timilifu.
“Progamu hii katika awamu ya kwanza imetekelezwa katika mikoa 10 ambayo ni Arusha, Dar Es Salaam, Dodoma, Kagera, Manyara, Morogoro, Lindi, Mbeya, Rukwa na Tabora na washiriki katika mikoa walipata mafunzo, kuanzia Aprili 2023 programu hii ilipanua wigo kwa kuongeza mikoa 16 iliyokuwa imebaki na kufikia mikoa 26,”amesema Kabuye.
Amesema katika utekelezaji wa programu hiyo jumla ya vituo 2341 vya kulele watoto mchana vimesajiliwa nchini vinavyohudumia watoto 17492 sambamba na uanzishwaji wa vituo vya kijamii 65 katika mikoa ya Dar Es Salaam, Dodoma na Tanga.
Naye Mwakilishi wa shirika la kuhudumia watoto Duniani (UNICEF) Mlemba Abassy, ambaye ni mtawimu, amesema kutokana na utafiti kuwa mchache wataendelea kushirikina na TAMISEMI, ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) pamoja na wadau wengine ili kupata viashiria vingi kuhusiana na malezi, makuzi a maendeleo ya awali mtoto.
Meneja Mradi wa Mtandao wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Lazaro Ernest, amesema kuwa Sayansi ya malezi inaeleza kuwa umri wa mwaka sifuri hadi miaka nane ndiyo kipindi sahihi cha kuwekeza katika malezi na makuzi ya mtoto.
“Katika kipindi hicho ndipo ubongo wa mtoto unakuwa kwa kasi hivyo ni wakati muhimu kuwekeza katika malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.”