Na. WAF – Dar Es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewaasa wazazi na walezi nchini kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ya Dini ikiwemo kuwasomesha Qur’an sambamba na kusoma Elimu ya Sekula/Dunia ili kuweza kuishi kwa kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu kama inavyoelekezwa kwenye Qur’an Tukufu na Hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W.)
Waziri Ummy ametoa wito huo leo Machi 17, 2024 akimuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika fainali ya Mashindano ya Ishirini na Tatu ya Kuhifadhi Qur’an Tukufu Kitaifa yaliyoandaliwa na Taasisi ya Aisha Sururu yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar Es Salaam.
“Tuwape watoto wetu muda wa kusoma Qur’an, tusiishie tu kuwakazania kwenda ‘tuitions’ za Elimu Dunia, tuwakazanie pia kwenda Madrasa ili waijue Quran, wamjue Mungu wao na kutengeneza maisha yao mema ya hapa Duniani na baada ya hapa Duniani.” Amesema Waziri Ummy
Amesema, Quran ni kitabu chenye fadhila kubwa sana na ndani ya Qur’an Tukufu kuna elimu kubwa na ya kutosha ambayo inapelekea watoto wetu au wasomi wengine kufuata matendo na maadili mema ambapo kuna elimu na hadithi za Bwana Mtume Mohammad (SAW) ambayo inapelekea nchi kuwa na utulivu, Amani na nidhamu katika jamii.
Waziri Ummy amenukuu Sura Al-Baqara aya ya 2 inayosema “Hiki ni kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake, ni wongofu kwa wacha Mungu”. Na pia Sura ya 96 inayohimiza watu kusoma “Soma kwa jina la mola wako alieumba; ameumba mtu kwa pande la damu; Soma! Mola wako ni karimu zaidi”.
Pia Mhe. Ummy amenukuu Sura Al-Araaf aya ya 204 inayosema “Na inaposomwa Qur’an basi isikilizeni kwa makini na bakieni kimya inaposomwa Qur’aan (Mzingatie) ili mpate kurehemewa.
Mhe. Ummy ameipongeza Taasisi ya Aisha Sururu kwa kuandaa mashindano hayo yaliyoshirikisha vijana zaidi ya 600 kutoka Mikoa yote ya Tanzania na amewashukuru Wadhamini wote waliofanikisha jambo hilo na kuwataka kutoacha kudhamini mashindano haya.
Vilevile, Waziri Ummy ametumia hadhara hiyo pia kutoa wito Kwa Watanzania kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kuepuka magonjwa Yasisyoambukiza ikiwemo Kisukari na Shinikizo la Juu la Damu (Presha) kwa kupunguza matumizi ya sukari, chumvi na mafuta pamoja na kufanya mazoezi.
“Tukizingatia hayo mambo makubwa Matatu, kupumguza matumizi ya sukari, chumvi pamoja na mafuta tutajiepusha na magonjwa mbalimbali Yasiyoambukiza kwa maana magonjwa haya yanaongeza kila siku na yanagharama kubwa sana kuyatibu.” Amesema Waziri Ummy.