Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed akizungumza na wananchi mjini Songea
Na Albano Midelo,Songea
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewatahadharisha watu watakaomletea majungu ofisini kwake ataweka loudspeaker kwenye simu kwa kuwa hana kifua cha kusikiliza na kuweka majungu.
Kanali Abbas ametoa tahadhari hiyo wakati anazungumza na watumishi ,viongozi na wananchi waliojitokeza kumsikiliza baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas.
“Sina utamaduni wa kusikiliza historia za nyuma ukiniletea majungu nitaweka simu loudspeaker kwa mtu unayempiga majungu ,sina kifua cha kusikiliza na kuweka majungu alisisitiza Kanali Abbas.
Amempongeza aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas kwa kusimamia vema miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa ambapo amesema yupo tayari kuwatumikia wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuanzia alipoishia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Ruvuma.
Ameahidi kutekeleza maagizo ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika Mkoa wa Ruvuma ambapo ametoa rai kwa viongozi na wananchi kushirikiana kwa kufanya kazi kama timu ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Naye aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza baada ya kukabidhi ofisi amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa na hatimaye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Kanali Thomas pia amewashukuru watumishi na wananchi wote wa Mkoa wa Ruvuma kwa ushirikiano mkubwa waliompatiwa wakati anatekeleza majukumu mbalimbali yakiwemo ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ametoa rai kwa watumishi wa Mkoa wa Ruvuma kutoa ushirikiano kwa Mkuu wa Mkoa aliyehamia ili aweze kutekeleza vema majukumu ya kuwahudumia wananchi.
Kanali Ahmed Abbas Ahmed anakuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wa 22 tangu kuanzishwa kwa Mkoa wa Ruvuma mwaka 1963.