Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imemuagiza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuimarisha vitengo vya Usimamiaji na Ufuatiliaji ili Mradi ya Ujenzi wa Shule itekelezwe kikamilifu kwa kuzingatia thamani ya fedha inaendana na ubora wa majengo.
Maagizo hayo yametolewa na Makamu Mwenyekiti wa PAC, Mheshimiwa Japhet Hasunga(Mb) mara baada ya Kamati kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Shule ya Wasichana ya Solya iliyopo Kata ya Kilimatinde Wilaya ya Manyoni, Mkoani Singida.
Mheshimiwa Hasunga amesema kukosekana kwa umakini wa usimamizi na ufuatiliaji wa miradi kunapelekea majengo kukosa ubora.
“Kamati tunaagiza TAMISEMI muongeze umakini katika usimamizi ufuatiliaji wa hii miradi ya ujenzi wa Shule, tunataka thamani ya pesa iendane na ubora wa majengo na miundombinu mingine.” amesema Mheshimiwa Hasunga
Mheshimiwa Hasunga aliongeza kuwa kukosa umakini katika usimamizi kunasababisha kuchelewa ukamilikaji wa miradi jambo linalopelekea kongeza gharama kwa serikali.
Aidha, Mheshimiwa Hasunga ameushauri uongozi wa Wilaya ya Manyoni kushirikiana na Wilaya zote za Mkoa wa Singida katika ujenzi wa shule hiyo kwasababu inahudumia Mkoa wote.
“Shule hii niyamkoa mzima wanufaika ni Mkoa mzima ndio maana kwenye taarifa nimesikia kila Wilaya ndani ya Mkoa wa Singida wamechagua wanafunzi kumi na mbili (12) bora wenye wastani wa alama A ndio wameletwa hapa kwaiyo naomba niwashauri Manyoni Swala hili sio la Manyoni Peke yake ni Mkoa mzima Shirikisheni Wilaya zote ndani ya Mkoa Mkamilishe Shule hii Kwa asilimia mia.” amesema Mheshimiwa Hasunga.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI(Miundombinu) Mhandisi Rogatus Mativila ameiahidi PAC kuongeza nguvu katika usimamizi wa miradi ya ujenzi wa Shule inayotekelezwa na Wizara hiyo ili kuhakikisha ubora na inakamilika kwa wakati.