Na Issa Mwadangala
Kauli hiyo ilitolewa Machi 14, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Theopista Mallya alipokuwa akitoa elimu juu ya madhara ya kutokufuata mila na desturi za nchi.
“Mnatakiwa kufuata mila na desturi zetu ikiwa ni pamoja kwenda kuabudu kwenye nyumba za ibada kila mmoja kwa imani yake na kuachana na mambo ya kishirikina ambayo hupelekea kufanya vitendo vya ukatili wa kijinsia na uhalifu ambavyo matokeo yake ni vifo” alieleza Kamanda Mallya
Pia, aliwataka wanafunzi kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi ambapo alibainisha kuwa jukumu lao ni kusoma na si kujihusisha na vitendo hivyo.
“Mwanafunzi akiwa shuleni ni kusoma tu, pia jiepusheni na lift za bajaji au pikipiki kwani baadhi ya madereva hao hushiriki kufanya ukatili kama ubakaji na ulawiti na wao wanapotea kwasababu hivyo vyombo sio vyao kwahiyo mnapaswa kuwa makini sana na lift au mkipanda pikipiki chagueni watu mnaowafahamu” Aliongeza SACP Mallya.
Vilevile alikemea tabia za baadhi ya wanafunzi kuzurula mitaani baada ya kutoka shuleni jambo ambalo wahalifu wa vitendo vya udhalilishaji hutumia muda huo kuwadhalilisha.
Hata hivyo amewataka wanafunzi hao kutoa taarifa za vitendo au viashiria vya udhalilishaji kwa mwenyekiti wa kijiji, kwa walimu wa malezi, kwa viongozi wa dini, kwa wazazi/walezi na Polisi ili taarifa hizo zishughulikiwe kwa haraka.
Baada ya elimu hiyo wanafunzi hao waliuliza maswali ambayo yalijibiwa na Kamanda Mallya pamoja na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Kutoka ofisi ya upelelezi Wilaya ya Momba Sadam Kitembe kwa kutumia vifungu vya sheria pamoja na vifungu vya Biblia.
Kwa upande wake, Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Iman Kamwela alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kutoa elimu katika shule yao na kuwataka wanafunzi wazingatie yale yote waliyofundishwa kipindi wawapo shuleni na nyumbani ili waweze kutimiza malengo yao katika masomo na maisha yao ya baadae.
Katika kikao hicho Kamanda Mallya aliambatana na Polisi kata wote wanaohudumu katika kata za Wilaya hiyo ili kusikiliza changamoto zinazowahusu na kutafutia ufumbuzi wa haraka.