Ikiwa ni katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, wafanyakaz Shirika la BRAC Tanzania Finance Limited (BTFL) wameshiriki katika matendo ya huruma kwa kutoa misaada katika maeneo mbalimbali nchini.
Meneja wa Mawasiiliano, Emma Mbaga amesema kuwa matendo haya ya huruma ni mpango wa wafanyakazi na kampuni ya BRAC ikiwa ni jitihada za kuchangia kumuinua mwanamke kiuchumi.
“BRAC ni shirika ambalo limelenga kuwakomboa wanawake kiuchumi na kijamii katika kila huduma ambayo tunatoa tukiamini wanawake ndio chachu ya maendeleo kuanzia ngazi ya familia na jamii nzima,”
“Wafanyakazi wa BRAC kila siku katika kazi zao wamekuwa wakishiriki katika kumkomboa mwanamke na kutoa fursa za kujiendeleza kufikia malengo yao. Hivyo basi Siku ya Wanawake duniani ni siku muhimu kwetu na kama wafanyakazi tunafurahia kuadhimisha kwa kuwafikia wanawake wenzetu na makundi mengine yenye uhitaji na kujitolea kile tulichonacho.”amesema Mbaga
Wafanyakazi wa BRAC nchini kote walitumia siku ya wanawake duniani kutembelea makundi ya watu wenye mahitaji maalum wakiwemo Watoto wanaoishi katika mazingira magumu, wafungwa wakike, wanawake na Watoto walio hospitalini ili kutoa misaada mbali mbali ikiwemo vyakula, mahitaji ya vyombo vya usafi n.k.
BRAC Tanzania Finance limited inaendesha shughuli za utoaji wa huduma ndogo ndogo za fedha kupitia matawi 177 yaliyo katika mikoa 23 nchini kote.
BTFL imeendelea kujivunia kuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma zinazolenga kukomboa wanawake kiuchumi kupitia huduma ndogo ndogo za kifedha za mikopo ikiwa na wateja zaidi ya 350,000 na zaidi ya asilimia 98 wakiwa ni wanawake.