Wakati Tanzania inaungana na mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Figo Duniani leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dkt. Alphonce Chandika, amewashauri wananchi kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kulinda figo zao.
Dkt. Chandika, ametoa wito huo jijini Dodoma, akisema wananchi wanapaswa wafanye mazoezi kuzingatia mlo usioathiri moyo ili kuzilinda figo.
“Mtindo bora wa maisha unaozingatia milo isiyoathiri moyo utaisaidia kuzilinda figo,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali.
Siku ya Figo Duniani mwaka huu inaadhimishwa ikiwa na kauli mbiu, ‘Afya ya Figo kwa Wote pamoja na Upatikanaji
Bora wa Matibabu.’
Dkt Chandika amesema wagonjwa 50 wenye tatizo la figo husafisha damu kwa siku katika Kitengo cha Kusafisha Damu katika Idara ya Magonjwa ya Figo katika BMH.
“Watu wenye tatizo la figo wanasafisha damu mara tatu (3) kwa wiki,” ameongeza.
Dkt Chandika amesema mpaka sasa, BMH imeishafanya oparesheni za upandikizaji figo kwa watu 36 toka huduma hii ianze miaka sita (6) iliyopita.
Mwaka 2019, BMH ilikuwa Hospitali ya pili nchini kuanzisha huduma ya upandikizaji figo, lakini ndiyo Hospitali pekee kutoa huduma hiyo bila usaidizi wa Hospitali za nje.