Serikali imepongeza na kushukuru mashirika binafsi kwa kuendeleza mapambano dhidi ya kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji katika jamii hasa kwa kundi la watoto wadogo na vijana
Hayo yamesemwa na kaimu afisa michezo wa manispaa ya Ilemela Mwalimu Maghembe Masalu wakati wa ufunguzi wa mashindano ya michezo ya mpira wa miguu kwa wasichana wa shule za msingi za kata za manispaa hiyo yaliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Plan International kwa lengo la kuwakutanisha watoto pamoja kujadili changamoto zao, kujitambua na kushiriki masuala ya elimu ambapo amefafanua kuwa uwepo wa mashindano hayo yatawajengea wanafunzi uwezo wa kujiamini na kuweka wazi vitendo vya ukatili vinavyoweza kujitokeza dhidi yako ikiwa ni pamoja na kuyatumia masanduku ya kutolea maoni yaliyopo katika shule zao kama sehemu ya kufichua vitendo hivyo
‘.. Kupitia mashindano haya pia watafundishwa vitu vingi hata kutambua ukatili na masuala ya wao kujitambua na kutoa maoni, Kwahiyo lazima tuwashukuru wadau wetu kwasababu wanatusaidia kuwajengea uwezo wasichana wetu kujielewa, Na kazi hii ilipaswa kufanywa na Serikali lakini wadau wakaona watusaidie, kwakweli tunawapongeza sana..’ Alisema
Aidha Mwalimu Maghembe ameyataka mashirika mengine kuiga mfano wa Plan International katika kubaini changamoto zilizo ndani ya jamii na kuzitafutia ufumbuzi badala ya kusubiria serikali pekee kufanya hivyo
Kwa upande wake mratibu wa mradi wa VEMA unaotekelezwa ndani ya manispaa ya Ilemela kutoka shirika la Plan International Bwana Gadiel Kayanda amesema kuwa mradi huo unasimamia vijana, malezi na ajira na utafanya kazi katika maeneo makuu matatu ikiwemo kuimarisha elimu, ulinzi wa mtoto na kuwezesha vijana kiuchumi
Kayanda meongeza kuwa wanashindanisha timu kutoka shule nane za kata ya Kayenze na Sangabuye kwa kuwa kata hizo zipo pembezoni mwa mji pamoja na kukabiliwa na changamoto ya idadi kubwa ya watoto kupata mimba na kuacha shule na wengine kujiingiza katika ajira za ndani na hatarishi wakiwa katika umri mdogo hivyo kupitia mashindano hayo wazazi na walezi watahamasika na kuwaruhusu watoto wa kike kushiriki masuala ya elimu
Nae mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nyafula Bi Laurencia Mapombe Elias amesema kuwa uwepo wa mashindano hayo katika shule yake yataongeza chachu ya wanafunzi kuhudhuria masomo pamoja na mshikamano kwa shule za kata hizo sambamba na kuishukuru Plan kusaidia uboreshaji wa miundombinu ya elimu ikiwemo ujenzi wa vyoo na madarasa
Anna Samuel ni mwanafunzi wa shule ya msingi Nyafula yeye ameshukuru uanzishwaji wa mashindano hayo huku akiwataka wazazi na walezi kuruhusu watoto wao kushiriki pamoja na kutowazuia watoto wa kike kupata haki ya kusoma