Mkurugenzi wa kamisehni ya kukabiliana na maafa Zanzibar Makame Khatib Makame akielezea mikakati waliyojiopangia kuelekea mvua za masika 2024 wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za kukabiliana na maafa Maruhubi Zanzibar.
Kaimu Mkurugenzi mamlaka ya hali ya hewa Tanzania kanda ya Zanzibar Masoud Makame Faki Akitoa mwelekeo wa mvua za masika kwa mwaka 2024 wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za kukabiliana na maafa Maruhubi Zanzibar.
Mtaalamu wa hali ya hewa kutoka mamlaka ya hali ya hewa kanda ya Zanzibar Hassan Khatib Ame akielezea hali ya El -Nino kwa mwaka 2024, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za kukabiliana na maafa Maruhubi Zanzibar.
PICHA NA FAUZIA MUSSA- MAELEZO ZANZIBAR
Na Ali Issa – Maelezo
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kanda ya Zanzibar imewataka wananchi kuchukua tahadhari kutokana na mvua za masika zilizo aza kunyesha hivi karibuni Nchini.
Hayo yamesemwa leo Maruhubi na kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Hali ya Hewa kanda ya Zanzibar Masuod Makame Faki wakati alipokua akitoa taarifa kwa wandishi wa Habari juu ya ujio wa Mvua za masika mwaka huu.
Amesema mvua hizo ambazo zimeendelea kunyesha kwa wiki ya pili katika maeneo mbali mbali ya visiwa vya Zanzibar ziatarajiwa kuisha katika wiki ya tatu ya mwezi wa mei 2024 kwa kiwango cha wastani na juu ya wastani.
Akizungumzia athari ambazo zinaweza kujitokeza alisema kuwa vipindi vifupi vya mvua kubwa zinaweza kujitokeza na kusababisha mafuriko, magonja na athari mbalimbali, hivyo ameitaka jamii kuchukuwa tahadhari mapema,
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Ndugu Makame Khatib Makame amesema kamisheni hiyo inaendelea na mikakati yake ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi ili kuchukua tahadhari mapema ya kujikinga na athari za Mvua hizo.
Aidha, amewataka Wavuvi na watumiaji wa bahari kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kuzifanyia kazi ili kuepukana na maafa yanayoweza kujitokeza wakiwa katika shughuli zao.
Vile vile, amewataka wananchi wanaoishi sehemu hatarishi ikiwemo pembezoni mwa Mito na kwenye njia za Maji kuchukua tahadhari mapema kabla ya kufikwa na maafa katika maeneo yao.