Viongozi wa wafanyakazi wanawake N,H,C wakifurahi na watoto katika kituo cha Beckhoff kilichopo katika Manispaa ya Mpanda.
Na. Zillipa Joseph, Katavi.
Wanawake wa makundi mbalimbali mkoani katavi wameadhimisha wiki ya wanawake kwa kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo kuonesha matendo ya huruma kwa makundi ya watu wenye uhitaji.
Wanawake kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wametoa msaada wa vitu mbalimbali kikiwemo chakula, sabuni na vifaa vya matumizi ya watoto vyenye thamani ya shilingi milioni mbili katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Beckhoff kilichopo Nsemulwa katika manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Afisa Habari wa Shirika la Nyumba la Taifa Bi. Domina Rwenyamula amesema katika kusheherekea sikukuu ya wanawake wameamua kutoa msaada kwa watoto wanaoishi katika kituo hicho ili kupunguza changamoto walizonazo.
Ameongeza kuwa watoto hao wanahitaji upendo kwani ni wazazi wa kesho.
Akitoa shukurani kwa niaba ya kituo hicho chenye jumla ya watoto 28 msimamizi wa kituo Sista Rose Sungura amewashukuru wanawake wa Shirika la Nyumba kwa kufika kuwaona na kwamba msaada huo utawasaidia kwa kiasi kikubwa.
Katika hatua nyingine wanawake kutoka Chama cha wafanyakazi wa serikali za Mitaa TALGWU mkoa wa Katavi wamefika katika gereza la mahabusu la mjini Mpanda na kutoa msaada kwa wafungwa wa kike waliopo katika gereza hilo.
Bi. Angela Ntemu ni Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa serikali za mitaa mkoa wa Katavi, amesema lengo la ziara yao hiyo katika magereza ya Mpanda ni pamoja na kuwatia moyo wanawake wanaoshi katika gereza hilo.
Pamoja na vitu walivyopeleka katika gereza hilo ni taulo za kike, na vifaa mbalimbali vya wanawake wanaotarajia kujifungua wakiwa gerezani kama vitenge na mabeseni.