Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya alipandishwa cheo kutoka Kamishna Msaidizi wa Polisi hadi kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, hivyo tunaomba mtmie picha hizi mpya.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Dainess Paul Mwashambo [30] mkazi wa Kijiji cha Mashese halmashauri ya Mbeya vijijini anayetuhumiwa kuwanywesha sumu ya kuulia magugu shambani watoto wake wawili, Mario Semen Adamson [4] na mdogo wake wa kike aitwaye Beonis Semen Adamson [2] wote wakazi wa Mashese ambapo walipoteza maisha walipofikishwa Hospitali.
Awali Machi 05, 2024 mtuhumiwa Dainess Paul Mwashambo [30] akiwa nyumbani kwake Kijiji cha Mashese – Ilungu aliwanywesha sumu ya kuulia magugu aina ya “Pare Force” watoto wawili na kusababisha vifo vyao muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya kwa matibabu.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni msongo wa mawazo uliosababishwa na kutuhumiwa kwa matukio ya wizi na serikali ya Kijiji cha Mashese. Mtuhumiwa baada ya tukio hilo naye alikunywa sumu hiyo na kwa sasa anaendelea na matibabu Hospitali ya Mkoa wa Mbeya chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, linatoa wito kwa jamii kuwa pindi unapopatwa na tatizo suluhisho lake sio kujichukulia sheria mkononi bali ni kutafuta ushauri au kufuata sheria inavyoelekeza ili kuepuka madhara kwako na jamii inayokuzunguka.
Imetolewa na:
Benjamin Kuzaga – SACP
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.