Nchini Tanzania na duniani kote, wanawake na wasichana wanakabiliwa na changamoto za usawa wa kijinsia ambao unachangia kuongeza hatari ya magonjwa, ulemavu, unyanyasaji wa kijinsia na vifo. Lengo la tano la Mendeleo Endelevu la Umoja wa Mataifa linalenga katika kufikia usawa wa kijinsia. Tunaposherehekea Siku ya Kimataifa ya Wanawake, inayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka, mataifa yote yanakumbushwa kuadhimisha mafanikio ya kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa ya wanawake katika kukuza usawa wa kijinsia na haki za wanawake duniani kote.
Tunapowazungumzia wanawake hususani wenye ulemavu wana uwezekano mara tatu zaidi wa kutopata huduma za afya wanazohitaji ikilinganishwa na wanaume wenye ulemavu. Na kwa wanawake wengi, kushughulikiwa kwa masuala yao ya afya hakujapewa kipaumbele katika orodha ndefu ya changamoto na vipaumbele vinavyokabili wanawake.
Siku hii ya Kimataifa ya Wanawake, Ijumaa tarehe 8 Machi, shirika la maendeleo la kimataifa la Sightsavers linatoa wito kwa huduma zote za afya ziwe jumuishi na zipatikane kwa wanawake na wasichana wote, wakiwemo wale wenye ulemavu.
Sightsavers pia inasherehekea, inawatambua na kuwapongeza wanawake wanaojitahidi kufanikisha hili.
Daktari Msaidizi wa kike wa magonjwa ya macho na upasuaji wa mtoto wa jicho Dk Upendo Mwakabalile anashirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kutoa huduma za afya ya macho kwa wagonjwa wakiwemo wanawake wenye ulemavu. Amekuwa akifanya kazi kama daktari wa upasuaji wa mtoto wa jicho tangu mwaka 2018. Anafanya kazi na mashirika ya kimataifa kama vile Sightsavers na Kilimanjaro Center for Community Ophthalmology kutoa huduma za matibabu ya macho katika jamii hasa maeneo ya vijijini mkoani Singida. Daima hupata fursa ya kupeleka huduma mkoba za upasuaji katika maeneo ya mbali zaidi ili kuhakikisha watu ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za usafiri, ikiwa ni pamoja na wanawake wenye ulemavu, wanaweza kufikia vituo vya afya na kupata huduma bora za macho zinazohitajika. Wakati wa huduma za uhamasishaji, anaona kuwa ukosefu wa usawa wa kijinsia ni suala la kimataifa na linatokea pia katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Singida.
Anasema, “Awali, Wagonjwa walipogundua daktari wa upasuaji ni mwanamke, waliogopa kufanyiwa upasuaji, na kusubiri kuona wanaotoka kwenye upasuaji kama wamefanikiwa, ndipo wanakubali niwafanyie upasuaji”. Hii ilimpa motisha ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuthibitisha kwa jamii kuwa wanawake ni wanaweza kufanya kazi mfano ya Udaktari sawa na wanaume.
Miongoni mwa mafanikio mengine, Dk Upendo alipokea Tuzo ya ‘Mtaalamu Bora’ inayotolewa na Shirika la Kimataifa la Kuzuia Upofu (IAPB) kutokana na mchango wake katika kujitolea kuokoa watu kutokana na upofu unaoweza kuepukika kwa kufanya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa wote wanaohitaji upasuaji. Pia alikuwa akitoa ushauri na elimu juu ya huduma itakayotolowa ili kujenga mahusiano mazuri kati ya daktari na mgonjwa kabla ya kufanyiwa upasuaji. Amepokea maoni chanya kutoka kwa wagonjwa ambao wameboresha au kurejesha uoni.
Anaamini kuwa huduma za afya ya macho zinachangia katika kuepuka upofu na kuboresha hali ya maisha na kujitegemea hasa kwa wanawake wenye ulemavu. Dk Upendo alisema, “Upatikanaji wa huduma za afya kwa wanawake wenye ulemavu ni haki muhimu, na nitoe wito kwa wahusika wote, ikiwa ni pamoja na serikali, wadau wa maendeleo, na mashirika binafsi, kuungana katika kuondoa vikwazo vya kupata huduma za afya.
“Miundombinu fikivu, rasilimali watu waliofunzwa, na teknolojia itasaidia wanawake kupata taarifa na huduma sahihi na kutoa maoni yao katika kuboresha huduma hizo, hivyo kusababisha kupatikana huduma nafuu, zenye ubora na endelevu.”
Kwa wanawake wenye ulemavu, changamoto hizi huchangiwa na umri , viwango vya juu vya magonjwa, na ugumu wa kupata huduma za afya.
Sightsavers hufanya kazi na washirika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, ikiwa ni pamoja na wanawake na watu wenye ulemavu, kama vile matibabu dhidi ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele (Non Tropical Diseases – NTDs) na shughuli za matibabu ya macho, wakijiunga na wito kwa ulimwengu kuhamasisha ushirikishwaji kwa kauli ya “hakuna mtu yeyote kuachwa nyuma”. Sightsavers pia huhakikisha wanawake wanaweza kupata taarifa kuhusu masuala ya afya kama vile kupunguza maambukizi ya magonjwa na huduma za afya ya uzazi na watoto wachanga.
Godwin Kabalika, Mkurugenzi wa Sightsavers nchini Tanzania anasema: “Bila kuchukua hatua, wanawake wataendelea kuachwa nyuma katika huduma za afya, afya zao na nafasi zao za elimu na ajira kupunguzwa.”
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2019 hadi 2023), wakati wa utekelezaji wa mradi wa Afya Jumuishi ya Macho nchini Tanzania, Sightsavers imefanya tathmini ya ufikivu kwa vituo 16 vya afya na kukarabati vituo viwili kutoka Singida na Morogoro ili kuhakikisha vinafikika na watu wenye ulemavu.
Shirika pia limekusanya takwimu kuhusu makundi yaliyotengwa ili kupata picha ya jinsi watu wanavyopata huduma za afya ya macho. Takwimu hizi zinaonyesha matatizo ambayo wanawake wanakabiliana nayo katika kupata huduma za afya.
Vikwazo vinavyohusishwa na unyanyapaa, ukatili, umaskini na upatikanaji mdogo wa elimu, ajira na uwezo wa kufanya maamuzi huchangia ukosefu wa usawa wa afya miongoni mwa wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Sightsavers inashughulikia masuala ya usawa kwa huduma za afya ya macho ambazo ni jumuishi na endelevu na kuhimiza wadau wengine kujumuika katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa pamoja.
Sightsavers inaungana na serikali na wadau wote kuadhimisha siku ya mwanamke na kupendekeza kuwa na bajeti inayozingatia mahitaji ya kijinsia zaidi, wanawake kushiriki zaidi katika nafasi za uongozi, kuboresha takwimu zilizogawanywa kijinsia ili kuarifu mipango na maamuzi katika sekta zote.