HANDENI TANGA Na Mwandishi wetu
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) amemuelekeza Mkuu wa Polisi nchini IGP Camillius Wambura kuongeza fedha kwa ajili ya Ujenzi wa nyumba za Askari zaidi ya 25 watakao hudumu katika Kituo cha Polisi Msomera kilichopo Wilayani Handeni Mkoani Tanga.
Maagizo hayo aliyatoa Machi 6, 2024 wakati alipofanya Ziara ya Kikazi ya Kutembelea na Kukagua mwendelezo wa Ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Msomera na nyumba moja iliyokamilika ya Askari inayoweza kukaliwa na familia mbili ambapo pia amehimiza kufanyiwa usafi wa mara kwa mara ili kuepuka kuchakaa huku wakijiandaa kukamilisha baadhi ya ofisi za idara nyingine kwenye kituo hicho.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeleta fedha nyingi kwa ajili ya kujenga Kituo hiki cha Polisi cha Msomera akiwa na lengo la kuimarisha Ulinzi na Usalama wa raia na mali zao katika eneo hili, hivyo hatutamtendea haki kikibaki kuwa na hali ya uchafu kwani kufanya hivyo kunapelekea kumkatisha tamaa na sisi kama wasaidizi wake hatuwezi kukubali” Alisema Mhe. Sagini
Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga Mhe. Alberto Msando, alimshukuru Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini kwa kufanya ziara hiyo na kumuahidi kutekeleza yale yote aliyoyaagiza.