Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akizungumza na wananchi wa wilaya ya Mbulu mkoa wa Manyara alipokwenda kutoa hati kwa wamiliki wa ardhi.
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu mkoa wa Manyara Kheri James akizungumza wakati wa zoezi la kutoa hati milki za ardhi kwa wananchi wa wilaya hiyo lililofanywa na Naibu Waziri wa Ardhi Mhe, Geophrey Pinda tarehe 6 Machi 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akimkabidhi hati milki ya ardhi mmoja wa wananchi wa Mbulu katika mkoa wa Manyara alipokwenda kutoa hati kwa wananchi waliomilikishwa tarehe 6 Machi 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akiwa katika picha ya pamoja na wananchi aliowakabidhi hati katika wilaya ya Mbulu mkoa wa Manyara tarehe 6 Machi 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Na Munir Shemweta, MBULU
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewataka wananchi wa wilaya ya Mbulu mkoani Manyara kujitokeza kwa wingi kuomba maeneo yao ya ardhi kutambuliwa.
‘’Naomba muendelee kujitokeza kwa wingi ili maeneo yenu yatambuliwe na hii itasaidia sana wanachi wa Mbulu kutogombana katika masuala ya ardhi kwa kuwa kila mmoja atakuwa na hati yake’’. Alisema Mhe, Pinda
Mhe, Pinda ametoa kauli hiyo tarehe 5 Machi 2024 katika halmashauri ya mji wa Mbulu wakati wa zoezi la kutoa hati kwa wananchi waliotambuliwa kupitia mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha (KKK) akiwa katika ziara yake ya siku mbili mkoani Manyara.
Jumla ya wamiliki wa ardhi 68 katika wilaya ya Mbulu mkoa wa Manyara walikabidhiwa hati milki za ardhi zilizopatikana kupitia mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha (KKK).
“Kupima na kumilikisha ardhi katika maeneo yenu hakumnyang’anyi haki mwenye eneo na kinachofanyika ni kutambua eneo lako kama ni shamba lako litambuliwe na kama ni kiwanja kitambulike.
Ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Mbulu kutokana na wilaya hiyo kutokuwa na migogoro mikubwa ya ardhi na kubainisha kuwa iwapo maeneo yote ya wilaya hiyo yatapimwa migogoro ya ardhi itakwisha yenyewe.
Vile vile, Naibu Waziri wa Ardhi amewahimiza wananchi wa Mbulu kuchangamkia hati zinazotolewa kupitia mradi wa KKK huku akiitaka ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Manyara kuhakikisha inahamasisha wananchi kujua ubora na matumizi ya hati.
“Tunataka kuhakikisha mji wa Mbulu unapangwa vizuri na kuwa katika mandhari nzuri” alisema Mhe, Pinda
Sambamba na suala hilo, Mhe, Pinda ameelezea kuwa, uwepo wa Klinik za ardhi kwenye maeneo mbalimbali nchini ni sehemu ya juhudi za wizara yake kushughulikia migogoro ya ardhi.
Amemtaka Msajili wa Hati na Nyaraka wa mkoa wa Manyara kuhakikisha anaharakisha utoaji wa hati kwa wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu ili kuwaondolea usumbufu.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mbulu Kheri James aliipongeza wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kupeleka mradi wa KKK ndani ya wilaya yake mradi aliouelezea umesaidia maeneo ya wilaya hiyo kupangwa, kupimwa na kumilikishwa.
‘’Mpango wa upimaji na upangaji katika wilaya yetu umetufanya tufanye ziara kila kijiji na kata kuelimisha kukumbusha na kuhamamisha wananchi’’. alisema Kheri James
Amesema, kwa kufanya hivyo anaamini dhamira ya serikali mji huo unapimwa na kupangwa na kufanana na miji mingine inatimia huku thamani ya ardhi ikipanda na migogoro ya ardhi ya mipaka kuisha kwa kuwa kila mwenye kiwanja atakuwa na hati yake itakwisha