Katibu mtendaji baraza la sanaa sensa ya filamu na utamadini Dkt. Omar Abdalla Adam akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya hatua za kumfungia msanii Zuhura Othman Soud (ZUCHU) kufanya kazi za sanaa Zanzibar kufuatia kukiuka mila,silka na utamaduni wa kizanzibari, huko Ofisi za BASFU Mwanakwerekwe.
Mrajis Baraza la sanaa sensa ya filamu na utamadini Juma chum juma akifafanua hatua za kufungiwa msanii Zuhura Othman Soud (ZUCHU) kufanya kazi za sanaa Zanzibar katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ofisi za BASFU Mwanakwerekwe.
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR
Na Rahma Khamis Maelezo Zanzibar
Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar limemfungia Msanii wa Bongo Fleva Zuhura Othman Suod (ZUCHU) kwa muda wa miezi sita na kulipa faini ya shiling milioni moja za kitanzania kutokana na kuimba nyimbo zisizokuwa na maadili na maudhui mazuri kwa vijana wa kizanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari huko Ofisini kwake Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharib B’ Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dkt Omar Abdalla Adam amesema hatua hiyo imekuja baada ya kufanya onyesho la burdani katika Kijiji cha Kendwa huko Hoteli ya Kendwa Fullmoon Part na kuonesha ishara zisizo na maadili na kuvaa vazi la uchi kitendo ambacho sio kizuri pamoja na kuimba nyimbo zisizo na maadili jambo ambalo ni kosa kisheria.
Amesema kwa mujibu wa kifungu namba 8 (1),(d) cha sheria nambari 7 ya 2015 ya Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar, lina haki ya kumfungia msanii huyo kutokana na kukiuka sheria zilizowekwa za kuimba nyimbo zinazozingatia mila silka na Utamaduni wa Mzanzibari.
Katibu huyo amefahamisha kuwa msanii huyo hana usajili kwa hapa Zanzibar katika utendaji wa kazi zake na wala hana mashirikiano ya aina yeyote katika Baraza hilo hivyo Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar limemfungia Msanii huyo na kumtaka kufika Zanzibar kuomba radhi na endapo atakwenda kinyume na agizo hilo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha Katibu ameitaka jamii ya Kizanzibar kupuuuza na kutosikiza nyimbo za msanii huyo pamoja na kundi lake kwani kuendelea kuzisikiliza na kuimba nyimbo hizo ni kuharibu mila na utamaduni uliopo.
Nae Mrajisi wa Baraza hilo Juma Chuom Juma amesema kwa mujibu wa Ibara namba 8 (B) inalitaka Baraza kuchukua hatua kwa wasanii wanaokuja kuimba Zanzibar bila ya kufuata utaratibu uliyopo kwani kuna sheria na utamaduni wake hasa ukizingatia kwamba kipindi kinachokuja cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.