Na. WAF – Tanga
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kutoa takwimu sahihi za vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka Mitano, chini ya mwaka Mmoja pamoja na vifo vya watoto wachanga wenye umri wa chini ya siku 28.
Waziri Ummy amesema hayo leo Machi 5, 2024 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakufunzi 110 kutoka katika vituo 25 vinavyotoa huduma ya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni (CEMONC), Vituo hivyo huchangia asilimia 86 ya wajawazito wanaojifungua katika vituo 44 vya CEMONC katika mkoa wa Tanga.
“Tunataka kuona takwimu hizo za makundi hayo Matatu pamoja na takwimu za kina mama wajawazito tunakua na makundi Manne, kipaumbele chetu sasa hivi ni watoto wachanga, hatutaki kusikia mambo ya mtoto si riziki yamepitwa na wakati.” Amesema Waziri Ummy
Amesema, ni muhimu kuendelea kutoa mafunzo kazini kwa watoa huduma za Afya kwa kuwa taarifa zinaonesha kuwa kati ya vifo 100 vitokanavyo na uzazi vinavyotokea takribani asilimia 85 ya vifo hivi vina uhusiano na mapungufu ya ujuzi “skills incompetence” kwa baadhi ya watoa huduma za afya.
“Pia ni muhimu kuwajengea uwezo watoa huduma za afya wa kuanzisha maeneo ya kujifunzia kumzalisha mama mjamzito (skills learning corners) katika vituo vya kutoa huduma za Afya pamoja na jinsi ya kumhudumia mtoto mchanga.” Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amewataka wakufunzi hao kwenda kuwajengea uwezo wenzao waliobaki katika vituo kwa kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha ujuzi wa watoa huduma za Afya ya mama na mtoto hususani watoto wachanga.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ataendelea kuchukua hatua za kuboresha huduma za Afya ya Uzazi mama na Mtoto, kwa kuwa ni jambo ambalo lipo moyoni mwake kuokoa maisha ya wanawake wenzake na vichanga vyao. Hivyo mafunzo haya yatakuwa ya muda mrefu hayataishia hapa.” Amesema Waziri Ummy
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya Dkt. Felix Bundala amesema hadi kufikia Juni 2025 wamepanga kuwafikia wakufunzi 2,860 katika Mikoa yote 26 ili waweze kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi mama na mtoto.
“Tunaamini kwamba tukiendelea kuwajengea uwezo wakufunzi kutoka vituo vya kutolea huduma za Afya tutasaidia sana kupunguza vifo vya mama na mtoto hususani watoto wachanga.” Amesema Dkt. Bundala