Na Albano Midelo
SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Afya imetenga zaidi ya shilingi bilioni 6.57 kutekeleza mradi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Songea.
Fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi wa majengo mapya,ukarabati wa vyumba vya kutolea huduma za afya na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya kutolea huduma bora za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas anasema katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ya Afya imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa jengo wagonjwa wa nje (OPD).
“Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma napenda kutoa pongezi za dhati Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mabilioni ya fedha kutekeleza miradi ya afya hivyo kujali afya za watanzania wa Mkoa wa Ruvuma’’,anasema Kanali Thomas.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Songea Dr. Magafu Majura anayataja majengo yaliyokamilika kwa asilimia 100 kuwa ni ujenzi wa nyumba ya daktari,ujenzi wa jengo la radiolojia kwa ajili ya CT Scan,Digital X Ray na ukarabati wa wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU).
Dr.Majura anayataja majengo mengine ambayo yamekamilika kwa asilimia 100 kuwa ni ukarabati wa chumba cha tiba masafa (Telemedidicine), ununuzi wa vifaa kwa ajili ya majengo ya wagonjwa mahututi (ICU),jengo la dharura (EMD),maabara na radiolojia.
“Kutokana na ufinyu wa eneo la hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Songea,Mkoa uliona umuhimu wa kuwa eneo jipya lenye ukubwa wa hekari 270 katika Kata ya Mwengemshindo Manispaa ya Songea,ambako kumeanzisha ujenzi wa hospitali mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma’’,anasema Dr.Majura.
Analitaja jengo muhimu ambalo wameanza nalo ni la wagonjwa wa nje (OPD) ambapo anasema mradi wa jengo hilo unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 3.8 ambapo hadi sasa jengo limefikia asilimia 71.
Akizungumzia jengo la radiolojia,Mganga Mfawidhi huyo anasema katika jengo hilo ndani yake kuna mashine mbili za CT Scan na Digital Xray ambazo zinafanya kazi na kwamba vifaa hivyo vina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili.
Anasema huduma za CT Scan zilianza kutolewa Machi 2023 hali ambayo imepunguza adha kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na mikoa jirani ambao awali walikuwa wanapata huduma hiyo katika hospitali ya Kanda ya Mbeya na hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya afya,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Louis Chomboko anasema katika kipindi cha mwaka 2023/2024 serikali imetoa shilingi bilioni 1.8 kutekeleza miradi ya afya katika hospitali za Halmashauri za Madaba na Manispaa ya Songea.
Anabainisha kuwa hospitali ya Halmashauri ya Madaba imepewa shilingi milioni 800,Halmashauri ya Manispaa ya Songea imepewa milioni 800 na kwamba shilingi milioni 200 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati za Ifinga,Likuyufusi,Litoromelo na Litindoasili.
Akizungumzia huduma za Afya ya uzazi na mtoto,Dr.Chomboko anavitaja vituo vinavyotoa huduma ya uzazi na mtoto vimefikia 348 kati ya vituo 419 sawa na asilimia 83 ya vituo vyote vinavyotoa huduma katika Mkoa.
Anabainisha kuwa vituo 325 sawa na asilimia 78 vinatoa huduma ya chanjo,kati ya vituo vya afya 50,vituo 17 sawa na asilimia 34 ya vituo vya afya vinatoa huduma kabambe za dharura za mama wajawazito na Watoto wachanga.
Kulingana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,kiwango cha akinamama waliojifungua kituoni kimeongezeka kutoka asilimia 84 mwaka 2022 hadi asilimia 87 hadi kufikia Desemba 2023.
Anasema vifo vya Watoto chini ya mwaka mmoja kwa mwaka 2023 vimeendelea kupungua kutoka 232 mwaka 2022 hadi vifo 131 mwaka 2023.
Akizungumzia hali ya utoaji chanjo,Dr.Chombo anasema kwa mwaka 2023 chanjo ya kifua kikuu imetolewa kwa asilimia 166,chanjo ya polio asilimia 135,chanjo ya dondakoo,kukakamaa na kifaduro zimetolewa kwa asilimia 135.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,chanjo ya kuzuia homa ya mapafu imetolewa kwa asilimia 135,chanjo ya kuzuia kuharisha asilimia 127,chanjo ya surua asilimia 152,chanjo ya pepopunda kwa wajawazito asilimia 106 na chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 ni asilimia 126.
Dr.Hussein Ngaila ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyasa anasema serikali imetoa zaidi ya bilioni tatu kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo ambao umefanyika kwa awamu tatu.
Anasema katika awamu ya kwanza serikali ilitoa bilioni 1.5 kujenga majengo saba ambayo ni jengo la utawala, mionzi, famasia,maabara,wagonjwa wa nje na huduma za mama na mtoto.
Kulingana na Dr.Ngaila awamu ya pili ya ujenzi ilihusisha majengo matatu ambayo ni wodi ya wanawake,wodi ya wanaume na wodi ya Watoto ambapo jumla ya milioni 490 zilitumika.
Katika awamu ya tatu serikali imetoa shilingi milioni 800 kujenga majengo manne ambayo ni jengo la upasuaji,wodi mbili za upasuaji kwa wanawake na wanaume,jengo la kuhifadhia maiti na ujenzi wa jengo la huduma za dharura (EMD) ambalo limegharimu shilingi milioni 300.
Naye Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Wilaya ya Tunduru Dr.Athumani Mkonoumo anasema serikali imetoa shilingi milioni 900 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa hospitali hiyo kongwe nchini iliyojengwa mwaka 1930.
Anasema fedha hizo zimejenga jengo la wagonjwa wa nje OPD,maabara na ukarabati mkubwa wa jengo la upasuaji na kwamba serikali imetoa shilingi milioni 300 kwa ajili ya jengo la huduma za dharura EMD.
Anasema serikali pia imetoa vifaa tiba kwa ajili ya jengo la EMD na hospitali ambavyo anavitaja kuwa ni mashine ya xray,ultrasound ya kisasa,mashine za kusaidia kupumua na mashine mbalimbali za maabara.
Dr.Chacha Wambura ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Madaba anasema serikali ya Awamu ya Sita pia imetoa zaidi ya shilingi bilioni tatu kutekeleza mradi wa ujenzi wa hospitali ya Halmashauri ya Madaba mradi ambao umekamilika na umeanza kuwahudumia wananchi.
Mkoa wa Ruvuma una vituo 419 vinavyotoa huduma za afya,kati ya vituo hivyo hospitali zipo 17,vituo vya afya 50 na zahanati 352.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas