Mkurugenzi wa fedha na Utawala wa TACAIDS CPA(T) Yasin Abas akiwasilisha mapendekezo ya kamati ya fedha wakati wa kikao cha Wadau cha Kujadili vyanzo Endelevu vya Mwitikio wa UKIMWI nchini.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Fedha Dkt Muhajir Kachwamba akichangia umuhimu wa upatikanaji wa vyanzo endelevu vya Mwitikio wa UKIMWI nchini wakati wa kikao cha wadau kilichofanyika jijini Arusha.
Dkt.Bonaveture Mpondo kutoka UNAIDS akiwasilisha mapendekezo ya kamati ya programe wakati wa kikao cha Wadau cha Kujadili vyanzo Endelevu vya Mwitikio wa UKIMWI nchini kilichofanyika jijini Arusha.
Wadau walioshiriki kikao cha Kujadili vyanzo Endelevu vya Mwitikio wa UKIMWI nchini kilichofanyika jijini Arusha anayezungumza ni Mratibu wa Mpango wa dharura wa Rais wa Marekeni wa Kudhibiti UKIMWI (PEPFAR) nchini Dkt Hiltruda Temba akichangia namna ambavyo nchi inaweza kuweka mikakati mizuri na kuweza kujitegemea katika Mwitikio wa UKIMWI.
Mwakilishi kutoka Shirikia la Kimataifa linaloshuhghulikia UKIMWI -UNAIDS Bw. Koech Rotich akizungumza na wadau namna ambavyo nchi inaweza kujipanga na kuweka vyanzo endelevu vya mwitikio wa UKIMWI nchini.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt Jerome Kamwela akitoa ufafanuzi kwa wadau namna ambavyo nchi imepiga hatua katika Mwitikio wa UKIMWI na namna inavyojipanga kuelekea kumaliza UKIMWI ifikapo 2030.
MKurugenzi wa Sera na Utafiti Bw.Godfrey Godwin akiwasilisha malengo ya kikao na mapendekezo ya kamati ya uongozi na utawala wakati wa kikao cha kujadili vyanzo endelevu vya mwitikio wa UKIMWI nchini.
…….
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania – TACAIDS kwa kushirikiana na wadau wamefanya Kikao cha Siku tatu Jijini Arusha kwa lengo la kufanya mafunzo, kujadili na kuweka mikakati endelevu kwa ajili ya mwitikio wa UKIMWI nchini.
Akizungumza katika Kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Jerome Kamwela amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika mwitikio wa UKIMWI, ambapo suala la uendelevu la raslimali za mwitikio wa UKIMWI limetajwa katika Sera ya UKIMWI ya mwaka 2001.
Dkt. Kamwela amefafanua kuwa Tanzania imekuwa moja ya nchi ambayo imepiga hatua kwa kuanzisha Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI, pia tayari imeanzisha Kamati ya Uendelevu wa Mwitikio wa UKIMWI, Tanzania imepokea Mwongozo wa Kimataifa wa Uendeshaji wa mpango huu, na kuwa na kamati ndogo za Fedha, Uongozi na Utawala, Programu na Jamii. Aidha, Dkt. Kamwela amesisitiza kuwa katika mwitikio wa UKIMWI ni suala mtambuka hivyo ni wajibu wa kila mdau kutekeleza wajibu wake, ili kufikia malengo ya Dunia ya kumaliza UKIMWI ifikapo 2030.
Naye, Mwakilishi wa UNAIDS Bw. Koech Rotich ametoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa iliyofanyika na kuleta mafanikio makubwa katika Mwitikio wa UKIMWI.
“Kazi inayofanyika hapa ni kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa mkoani Lindi mwaka 2022, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani. Suala la uendelevu la Mwitikio sio fedha pekee, bali ni kuangalia ni kwa namna gani tunapambana kumaliza UKIMWI ifikapo 2030 na mipango baada ya 2030. Ifikapo Disemba Mwaka huu tutawasilisha taarifa ya utekelezaji wa agizo hili, ambapo tutakuwa na mpango wa utekelezaji (road map), alisisitiza Koech”
Kwa upande mwingine Mratibu wa Mpango wa dharura wa Rais wa Marekeni wa Kudhibiti UKIMWI (PEPFAR) nchini, Bi. Jessica Greene ameipongeza TACAIDS na UNAIDS kwa hatua iliyofikia katika maandalizi ya mpango wa utekelezaji wa Uendelevu wa Mwitikio wa UKIMWI. Aidha, Bi Greene amesema kuwa matokeo ya Tanzania HIV Impact Survey (THIS) yanaleta matumaini makubwa na kutakiwa kujipanga kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa katika kutekeleza afua za UKIMWI na kujipanga kwa mipango ya baadaye. PEPFAR itaendelea kufanya kazi na Serikali, ili kuandaa na kutekeleza Uendelevu wa Mwitikio wa UKIMWI.
Aidha, washiriki wa kikao hicho wameeleza kuwa miongozo na mikakati ya nchi inayolenga kumaliza au kupunguza tatizo la UKIMWI, itaendelea kutoa kipaumbele kwenye suala la kuwa na chanzo endelevu cha rasilimali za UKIMWI, ili kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kupata chanzo cha kudumu cha rasilimali za Mwitikio wa UKIMWI.
Wadau wa maendeleo waliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali katika kuhakikisha Mpango wa kuimarisha upatikanaji wa chanzo endelevu cha rasilimali za UKIMWI na kusisitiza kuwa chanzo endelevu sio tu raslimali fedha, bali ni pamoja na njia nyingine zitakazo wezesha kumaliza UKIMWI ifikapo 2030.
Katika kikao hicho kuliwasilishwa hali ya UKIMWI, ambapo ilielezwa kuwa Tanzania bado haijafikia hatua nzuri katika malengo ya asilimia 95 ya kwanza ya kuhakikisha wanaoishi na Virusi vya UKIMWI wanafahamu hali zao, hivyo bado kuna haja ya kuhamasisha au kuweka mipango ya uhamasishaji jamii kupima na kujua afya zao. Hii ni pamoja na kuanza kutumia dawa.
Kikao hicho cha mafunzo na mjadala, kwa ajili ya Uendelevu wa Mwitikio wa UKIMWI, kimewashirikisha pia wadau na sekta zote zinazojumuisha shughuli zinazoweza kuchangia ongezeko la maambukizi ya VVU. Sekta hizo ni pamoja na madini, Sekta Binafsi, Kilimo, Ujenzi, Utalii na Sekta ya Usafirishaji. Aidha, Washiriki wameishukuru Serikali kwa jitihada zinazofanyika kuandaa mpango wa Uendelevu wa Mwitikio wa UKIMWI.
Kaimu Mkurugenzi wa TACAIDS Dkt Jerome Kamwela, amewashukuru washiriki wote kwa michango yao na ushirikiano walioutoa tangu mwanzo wa kikao hadi kumalizika kutokana na ushirikiano waliutoa.