KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,akikabidhi vifaa tiba vya watu wenye ulemavu vilivyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba Mhe.Zulfa Mmaka Omar.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,akikabidhi mifuko ya saruji iliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba Mhe.Zulfa Mmaka Omar.
NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, amesema CCM itatoa kipaumbele kwa Viongozi wa majimbo wanaotekeleza kwa ufanisi Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025.
Msimamo huo umeutoa wakati akikabidhi Vifaa vya ujenzi wa nyumba ya kitega uchumi na Ofisi za U.W.T Mkoa wa Kusini Pemba vilivyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba Zulfa Mmaka Omar huko Shehia ya Madungu.
Mbeto,alisema katika Uchaguzi wa mwaka 2025 kila kiongozi wa jimbo atapimwa na kutathminiwa utendaji wake wenye kuacha alama katika Chama na Jumuiya zake pamoja na ukaribu wao na Wananchi waliowapa ridhaa ya kuongoza.
Alisema ni CCM itaendeleza mikakati wake wa kufanya Siasa za Kisayansi za kutekeleza Sera kwa vitendo kuliko maneno na kutoa ahadi zisizotekelezeka.
Katika maelezo yake Mbeto,alitoa wito kwa Viongozi wote wakiwemo madiwani,wabunge na wawakilishi kujiandaa kisaikolojia kwa kubadilika kitabia kwa kurudi majimbo mwao kutekeleza ahadi zote walizoahidi na kwamba CCM haitokubali kuadhibiwa na Wananchi kwa makosa ya Viongozi hao.
“Viongozi fanyeni kazi mlizoomba kwa Wananchi kwani ndio tiketi ya kuwarudusheni madarakani,asiyefanya kazi huyo atakuwa haitoshi kwenda na sisi katika safari yetu ya kisiasa.”,alisema Mbeto.
Alimpongeza Mbunge huyo Mhe.Zulfa kwa kazi kubwa aliyofanya ya kutoa vifaa vya kujenga jengo la kisasa la Jumuiya ambayo kila mwanachama wa Mkoa huo atanufaika kutokana na huduma zitakazotolewa wakati jengo hilo litakapokamilika.
Aliwata wanachama na viongozi wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba kujiandaa kikamilifu na Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuhakikisha Chama kinashinda kwa ngazi zote.
Vifaa vya ujenzi vilivyotolewa ni pamoja na nondo 25,mifuko ya saruji 50,matofali,gari za mchanga na vifaa vya watu wenye ulemavu vyenye thamani ya shilingi milioni 9.5.