Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali inaendelea kufanya mageuzi ya Elimu, na kuboresha mbinu za ufundishaji kuanzia ngazi za Awali hadi Vyuo Vikuu ili kupata Wahitimu Mahiri kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Waziri Mkenda amesema hayo Februari 26, 2024 Mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) kukagua Mradi wa ujenzi wa majengo ya Maktaba na ukumbi wa mihadhara yanayojengwa kwa fedha za ndani kiasi.
“Katika kutekeleza mageuzi ya elimu tunatakiwa kuwa wabunifu katika ufundishaji na lazima tubadilike ili kuimarisha ubora wa elimu katika Vyuo Vikuu na nyanja zote za elimu kuanzia elimu ya awali ili mwanafunzi aweze kufanya vizuri zaidi”, Alisema Prof. Mkenda.
Waziri Mkenda amesisitiza kila Kitivo kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili kuwasaidia wanafunzi kufanya vizuri zaidi na kuendana na kasi ya mabadiliko ya elimu.
Aidha Prof. Mkenda amesema kuwa Serikali imetoa fedha za maboresho ya elimu kwa taasisi za elimu ya Juu nchini kupitia Mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi wa Elimu ya Juu (HEET) ambapo MoCU kimetengewa Dola za Marekani Milioni nane 8,000,000 ambazo zinatumika katika maboresho katika taasisi ya elimu ya Ushirika na Biashara ya Kizumbi iliyopo Mkoani Shinyanga.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU) Prof. Alfred S. Sife amesema Chuo hicho kinaendelea na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Jengo la maktaba na ukumbi wa mihadhara ambao ulianza Septemba 12, 2022 unatarajia kukamilika Septemba 11, 2024.
Prof. Sife amesema kuwa Mradi wa ujenzi wa majengo Matatu chuoni hapo, ambapo ni bweni lenye uwezo wa kuchukua Wanafunzi 1,154, Jengo la Taaluma (Academic Complex) lenye uwezo wa kuchukua 1,810 na Jengo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano lenye uwezo wa kuchukua Wanafunzi 460.