Katikati ni Chifu wa Tano wa Wangoni Nkosi Emanuel Zulu Gama akiwa ndani ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji
Na Albano Midelo,Songea
Utalii wa kiutamaduni hapa nchini bado haujapewa kipaumbele ukilinganisha na nchi nyingine kama Afrika ya kusini ambayo utalii huo umepiga hatua kubwa.
Mkoa wa Ruvuma una utajiri mkubwa wa utalii wa utamaduni ukilinganisha utalii wa ikolojia,miongoni mwa vivutio vya utalii wa utamaduni ni Makumbusho ya Taifa ya Majimaji yaliopo katika eneo la Mahenge Manispaa ya Songea ambayo yamesheheni utalii wa kihistoria na kiutamaduni.
Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anabainisha kuwa,wadau wa utalii katika Mkoa wa Ruvuma wamekusudia kuanzisha utalii wa kiutamaduni (cultural tourism) sanjari na kuboresha maeneo yote ya kihistoria ili kuendeleza utamaduni hatimaye maeneo hayo yaweze kuingiza mapato baada ya watalii kutembelea kama ilivyo katika visiwa vya Zanzibar.
Challe anasema,wadau kutoka wilaya zote za mkoa wa Ruvuma tayari wameshatembelea maeneo muhimu ya kihistoria kama vile Makumbusho ya Taifa ya Majimaji, Maposeni,Luhira na Chandamali katika Wilaya ya Songea ili kutambua maeneo ya kihistoria na umuhimu wake kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Huu ni mwanzo wa jukumu la kuziboresha kumbukumbu za kihistoria katika mkoa wa Ruvuma na kuimarisha utalii wa ndani na nje lengo likiwa ni kuutangaza mkoa wa Ruvuma kupitia sekta ya utalii wa kiutamaduni’’,anasema Bartazar Nyamusya Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji.
Nyamusya anasisitiza kuwa serikali imeyafanya Makumbusho ya Taifa Majimaji kuwa ya kitaifa kutokana na makumbusho hayo kuhifadhi vifaa na silaha ambazo walitumia mashujaa hao kupambana na wakoloni wa kijerumani.
“Hii ni Makumbusho pekee nchini ambayo imebahatika kuwa na vifaa vyote asilia na muhimu katika historia ya mtanzania hali ambayo inaitofautisha makumbusho hii na nyingine zilizopo hapa nchini ”,anasisitiza Mhifadhi huyo.
Naye Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Philipo Maligisu anabainisha zaidi kuwa Mji wa Songea ni miongoni mwa miji michache nchini ambayo ilitoa upinzani mkali katika vita ya majimaji na kwamba katika makumbusho hayo kuna ushahidi ambao unaonesha moja kwa moja kuwa wazee wa Songea walishiriki kikamilifu katika vita hivyo.
Anabainisha zaidi kuwa katika eneo la mashujaa wa majimaji yamejengwa majengo mbalimbali ambayo yamehifadhiwa vifaa ambavyo vilitumiwa na mashujaa hao ili kuwaletea watanzania uhuru.
Ndani ya makumbusho ya Taifa ya Majimaji kuna mnara wa kumbukumbu ya wanajeshi ambao walitoka Songea kwenda kupigana vita ya Idd Amini kati ya mwaka 1978 hadi 1979 ambapo wakati wanarudi baada ya kushinda vita walipata ajali mbaya na kufariki dunia askari wote 56 katika milima ya Lukumbulu wilayani Songea.
Ili kuwakumbuka mashujaa hao serikali ilijenga mnara katika eneo Makumbusho ya Taifa ya Majimaji ambako walizikwa mashujaa wa vita ya majimaji kama sehemu ya kuwakumbuka.
Kulingana na sera ya utamaduni ya mwaka 1997 pamoja na sheria ambayo inayatambua maeneo haya serikali imeamua mji wa Songea uingizwe katika vivutio vya utalii wa kiutamaduni kwa ajili ya kuendeleza historia ya Mji wa Songea ili uwe wa kihistoria, kishujaa na kiutamaduni.
Utafiti uliofanywa na Makumbusho ya Taifa umebaini kuwa mji wa Songea una vigezo vyote vya kuingizwa katika rasilimali za kiutamaduni za taifa,ili kuhakikisha kuwa watalii wengi wa ndani na nje ya nchi wanafika katika makumbusho hayo kujifunza mambo mbalimbali ya historia ambayo ni urithi wa taifa letu.
Kwa upande wake Chifu wa Tano wa Kabila la Wangoni Nkosi Emanuel Gama anasema kila mwaka Baraza hilo hufanya kumbukizi la kuwaenzi na kuwakumbuka mashujaa mashujaa 67 ambao walinyongwa na wajerumani na kuzikwa katika makaburi mawili ndani ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea.
Anasema katika tukio la mashujaa hao kunyongwa walitimiza wajibu wao kwa ajili ya maslahi ya taifa letu la sasa na kizazi kijacho ambapo ushujaa ndiyo njia pekee ya kujikomboa na kulinda uhuru wa Taifa letu.
Hata hivyo anasema hali ya mila,utamaduni na desturi iliyopo kwa vijana wa sasa katika nchi yetu ni mbaya kwa kuwa vijana wengi wamesahau utamaduni mila na desturi za mtanzania na kuendekeza mila za kigeni ambazo zimeharibu kabisa maadili mema ya mtanzania.
Mwaka 2024 Mkoa wa Ruvuma umefanya tamasha la kumbukizi ya miaka 119 ya mashujaa wa vita ya Majimaji wapatao 67 waliuawa kwa kunyongwa na wajerumani mwaka 1906.
Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wakiwa ndani ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji kujifunza utamaduni na historia ya harakati za ukombozi wa mtanzania tangu enzi za wakoloni