Mbunge wa Jimbo la Ilemela MNEC Mhe Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa mtaa wa Kabuhoro kata ya Kirumba wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero na changamoto za wananchi mtaa wa Kabuhoro kata ya Kirumba
……..
Wananchi wa mtaa wa Kabuhoro kata ya Kirumba wameaswa kutoa ushirikiano kwa mkandarasi Kones Construction anaejenga kipande cha barabara ya Kabuhoro-Ziwani chenye urefu wa mita mia saba na upana wa mita 6.5 kwa fedha za mfuko wa jimbo kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 262 kwa muda wa miezi sita
Rai hiyo imetolewa na mbunge wa jimbo la Ilemela (MNEC) Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa mkutano wake wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi uliofanyika katika viwanja vya Bujumbura mtaa wa Kabuhoro kata ya Kirumba ambapo amewataka kuondoa vikwazo visivyo vya msingi ili kurahisisha utekelezaji wa mradi huo na kukamilika kwa wakati na wananchi wa eneo hilo waweze kupata huduma
‘.. Hatua za manunuzi zimeshafanyika, mkandarasi ameshapatikana, mkataba ushasainiwa na wiki ijayo tutakuja hapa kumkabidhi site sasa asitokee mwananchi kwa sababu zake binafsi zisizo za msingi akakwamisha utekelezaji wa mradi huu, Tutakwama tusifanye hivyo tumpe ushirikiano tupate huduma ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa maendeleo ndani ya jimbo lake sanjari na kumtaka mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anatumia wananchi wa eneo hilo kwa kazi za vibarua wakati wa utekelezaji wa mradi huo
Kwa upande wake mhandisi Uswege Meshack Jacob kutoka taasisi ya wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA wilaya ya Ilemela mbali na kumpongeza mbunge Dkt Angeline Mabula kwa kupambania kuongezwa kwa bajeti ya taasisi yake kutoka bilioni 1.2, Na kuongezewa milioni 500 za kila jimbo, baadae kupokea bilioni 1 kutoka tozo za mafuta amewataka wananchi wanaoishi kando ya barabara hiyo kuandaa mazingira ya kuupokea mradi kwa kukata kwa hiari miti iliyo jirani na barabara ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima wakati wa ujenzi wa barabara hiyo
Mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Ndugu Kennedy Chigulu ambae pia ni afisa ardhi amesema kuwa manispaa yake imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kwaajili ya fidia kwa mwaka ujao wa fedha pamoja na kuwataka wananchi kutojenga maeneo hatarishi kwani upimaji shirikishi hauruhusiwi kufanyika kwa maeneo hayo kwa mujibu wa sheria huku akisisitiza ulipwaji wa kodi za ardhi ili Serikali ipate fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo
Juma Wesa ni diwani wa kata ya Kirumba pamoja na kueleza shughuli za maendeleo zilizofanyika katika kata yake, ameishukuru Serikali na kumpongeza mbunge wa jimbo hilo kwa ushirikiano anaompatia katika kuwatumikia wananchi wake huku akiwaomba wananchi hao kuendelea kukiamini chama chake na kuwachagua tena katika uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ili wazidi kuwaletea maendeleo