Mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro Nyerere akizungumza na mwananchi wa Kata ya Kirando wakati akijibu kero za wananchi hao.
Wananchi wa kata ya Kirando Kijiji cha Kirando wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Rukwa.
Na Gurian Adolf-Nkasi
MKUU wa mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere amewaagiza wakuu wa wilaya, Wakurugenzi, Maafisa Tarafa na Watendaji Kata kuhakikisha wanatatua kero za wananchi katika maeneo yao ili waendelee kuiamini serikali ya awamu ya sita.
Agizo hilo alilitoa hivi karibuni wakati akizindua Kliniki maalumu inayotembea ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi mkoani humo ambapo uzinduzi huo ulifanyika katika Kijiji cha Kirando kilichopo wilayani Nkasi.
Alisema kuwa wananchi wamekuwa na kero mbali mbali ambazo zinahitaji majibu lakini bahati mbaya hawapati watendaji wa kuwatatulia kero hizo hivyo ametoa siku 30 kwa watendaji wa serikali kutembea kwenye kila kata kwaajili ya kutatua kero za wananchi.
“kipimo cha utendaji wa kiongozi bora ni pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi kuna wakati wananchi wanailaumu serikali kwakua hakuna mtendaji anayetoa majawabu ya kero zao, hivyo nataka mfanye kazi hiyo ili wananchi wasije kuilaumu serikali ya awamu ya sita” alisema.
Akiwa katika uzinduzi huo, mkuu wa mkoa alipokea kero na malalamiko 20 katika Kata za Kirando na Itete na kuzipatia Majibu ambapo pia aliwaagiza watendaji hao kuhakikisha nao wanafanya kazi hiyo katika maeneo yao ili wananchi waishi kwa amani.
Naye Mwananchi aitwaye, Francis Sinkala aliyetatuliwa mgogoro wa ardhi baina yake na jirani yake alimshukuru mkuu wa mkoa Nyerere kwa kuanzisha Kliniki hiyo kwani itakwenda kuondoa baadhi ya changamoto zinazo sababisha malumbano na kukosekana amani baina ya wananchi.
Kwaupande wake Flaviana Michael mkazi wa Kirando aliomba Kliniki hiyo kuhakikisha inatua changamoto wanazokutana nazo wajawazito na watoto pindi wanapo kwenda kwenye vituo vya huduma za afya kupata matibabu hasa suala la matibabu bure kwani wanayokutana nayo ni tofauti na wanayoambiwa na viongozi wa serikali.