Na John Walter -Manyara
Wanafunzi zaidi ya 1,000 wa shule za msingi, sekondari na vyuo wilayani Babati mkoani Manyara wamepewa mafunzo maalum ya kudhibiti dawa za kulevya kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa hizo nchini (DCEA) Kanda ya Kaskazini.
Mamlaka hiyo imeamua kuwekeza katika kutoa elimu ya dawa za kulevya kwa wanafunzi ili kuwawezesha kutimiza ndoto walizonazo kwani kundi kubwa linalotumbukia kwenye matumizi ya dawa hizo ni vijana ambao wengi wao wapo mashuleni na vyuoni.
Afisa ustawi wa jamii kutoka mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya Kanda ya kaskazini Sarah Ndaba, amesema mafunzo hayo yametolewa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Manyara, wakiamini kuwa itakuwa chachu kwa wanafunzi, walimu na wananchi kwa ujumla kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na rushwa.
Wamefanya ziara ya siku tatu mkoani Manyara kutoa elimu kwa Wanafunzi 1000 wa shule za msingi, Sekondari na vyuo ikiwa ni ushirikiano waliouanza kupitia vilabu vya wapinga rushwa vilivyopo mashuleni na vyuoni ili viwe vinafanya kazi mbili ya kupinga rushwa na kupambana na dawa za kulevya.
Aidha Ndaba amesema kwa ukanda wa kaskazini ikujumuisha mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga kuna vituo tiba zaidi ya 26 kwa ajili ya kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya.
Afisa elimu jamii wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya (DECA) Shabani Miraji amesema dawa za kulevya zinaweza kusababisha madhara ya kiafya yakiwemo maradhi ya kuambukiza na yasiyoambukizi.
Miraji amesema katika vita hiyo ya kudhibiti matumizi na biashara ya dawa za kulevya, Mamlaka itaendelea kutoa elimu katika shule za Msingi, sekondari na vyuo mbalimbali mbalimbali na kwenye mikutano ya hadhara.
Naye afisa elimu wa TAKUKURU mkoa wa Manyara Richard Samila amesema waliingia makubaliano ya pamoja kuelimisha vijana wa vilabu vya wapinga ili kuwa na maadili mema kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa, matumizi na uuzaji wa dawa za kulevya.
Kwa upande wake mkuu wa chuo cha Veta Ghorowa Henry Kasele ameiomba DCEA na TAKUKURU wafanye mafunzo hayo mara kwa mara kwa kuwa waathirika wakubwa wa dawa za kulevya ni vijana ambao wengi wao wapo mashuleni na vyuoni.
Ameeleza kuwa elimu iliyotolewa chuoni hapo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwaepusha vijana kuingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya.
Nao Wanafunzi wa chuo cha ufundi Veta Ghorowa wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo waliahidi kuelimisha wengine juu ya athari za dawa za kulevya.