Serikali ya Tanzania inayo dhamira ya dhati ya kushirikiana na Marekani katika kukuza biashara na uwekezaji na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania na Marekani.
Vikevile, Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Chemba ya Wafanyabiashara wa Marekani-Tanzania (AMCHAMTZ) na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) ili kufanikisha malengo ya Mpango Mkakati wa AMCHAMTZ yaliyokusudiwa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Sempeho Manongi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hashil Abdallah wakati wa Uzinduzi wa Mpango Mkakati wa AMCHAMTZ ya Mwaka 2024 uliofanyika Februari 22, 2024 jijini Dar es Salaam
Aidha, Bw. Manongi amesema Mpango Mkakati huo unaolenga kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani ni hatua muhimu katika utekelezaji wa makubaliano ya “U.S.-Tanzania Commercial Dialogue” yaliyofikiwa na mawaziri wa biashara wa nchi hizo mbili.
Amebainisha Mpango huo unalenga kushughulikia vikwazo vya biashara, kuboresha sera, na kuongeza uwekezaji katika sekta muhimu kama vile nguo, ufundi, usindikaji wa chakula, na ngozi.
Naye Mwenyekiti wa AMCHAMTZ, Geofrey Mchangila amesema unalenga kuimarisha uwezo wa wafanyabiashara wa Tanzania, kuboresha mazingira ya biashara, na kuongeza ufikiaji wa masoko ya Marekani.
Uzinduzi wa Mpango huu wa AMCHAMTZ unatarajiwa kuchochea ukuaji wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani, na hivyo kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi wa nchi hizi mbili.