Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Dr. Alex Mrema (kulia) akizungumza na waandishi wa habari. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Tanganyika Shabani Juma.
Na. Zillipa Joseph, Katavi
Madakitari bingwa 18 kutoka nchini Marekani wanatarajiwa kuwasili Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi kwa ajili ya kutoa matibabu ya kibingwa.
Ujio wa madaktari hao bingwa utawasaidia wagonjwa walioshindwa kwenda kwenye matibabu ya rufaa nje ya mkoa kupata fursa ya kutibiwa.
Akizungumza na wanahabari Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tanganyika, Shabani Juma amesema halmashauri hiyo kwa kushirikiana na shirika la The Norbert and Friends Mission (NFM-BRIGHT) wanaleta madaktari hao bingwa wataokuja kwa makundi mawili ambapo kundi la kwanza litawassili Aprili 6 mwaka huu na kundi la pili litawasili Mei 4 mwaka huu.
Akizungumzia ushirikiano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la The Norbert and Friends Mission (NFM-BRIGHT), Joel Yalanda amesema lengo la shirika hilo ni kuisaidia Serikali kutotumia pesa nyingi katika kutoa matibabu.
“Kwa kutambua mzigo unaobebwa na Serikali yetu tumeona tushiriki pamoja katika kupunguzia mzigo Serikali kwa kutumia fedha nyingi kwenye upande wa upasuaji ambao imekuwa ni changamoto kwa jamii yetu”
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Dr. Alex Mrema amesema maandalizi ya kuwapokea wagonjwa yapo vizuri na katika kipindi chote cha uwepo wa Madaktari hao huduma zitakuwa zinaanza kutolewa kuanzia saa moja asubuhi hadi saa kumi na moja jioni.
“Huduma hizi za upasuaji kwa Halmashauri ya Tanganyika ni za muhimu kutokana na kwamba jiografia ya Halmashauri yetu ni kubwa lakini hakuna wataalamu wa upasuaji ndani ya Halmashauri yetu na wilaya yetu”
Madaktari hao, watatoa huduma kwa watoto na watu wazima bila malipo, na baadhi ya huduma hizo ni upasuaji wa uvimbe na saratani ya matiti, upasuaji wa eneo la tumbo, upasuaji wa uso na kichwa, upasuaji wa masikio, pua na koo na upasuaji wa Ini.
Dk. Mrema alitumia fursa hiyo kuwaalika wakazi wote wa mkoa wa Katavi kufika kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu bure.