Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa Kabuku Wilaya ya Handeni wakati akiwa ziarani mkoani Tanga tarehe 21 Februari 2024.
……
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Philip Mpango ameigiza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Tanga kuchukua hatua za mapema katika kukabiliana na changamoto ya soko la matunda yanayozalishwa mkoani humo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Kabuku Wilaya ya Handeni akiwa ziarani mkoani Tanga leo tarehe 21 Februari 2024. Ameuagiza uongozi wa mkoa wa Tanga kufanya tathimini na kutambua kiasi cha matunda yanayozalishwa katika eneo hilo.
Aidha Makamu wa Rais amemuagiza Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara kukutana na wamiliki wakubwa wa viwanda vya kuchakata matunda (Bakhresa na Jambo Product) ili waweze kutumia matunda yanayozalishwa Wilaya ya Handeni na Tanga kwa ujumla katika bidhaa zao.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Kabuku na Watanzania kwa ujumla kuongeza jitihada katika utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Amesema athari za uharibifu wa mazingira zimepelekea ongezeko la joto kupita kiasi, ongezeko la mvua ambayo imepelekea uharibifu wa miundombinu na mlipuko wa magonjwa.
Amesema ni muhimu watanzania kutambua uhifadhi ya mazingira ni jukumu la kila mmoja kwa kuacha kukata miti ovyo, kuacha kuchoma misitu pamoja na kupanda miti na kuitunza.
Makamu wa Rais amewasisitiza wananchi wa Kabuku kuhakikisha wanazingatia elimu kwa watoto ili kuwa na kizazi bora na chenye maarifa kwa manufaa ya Taifa. Pia amewaasa wananchi wa eneo hilo kuzingatia lishe kwa kuwa ndio msingi wa afya bora ya mwili na akili.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Wizara imepokea shilingi bilioni 25 kwaajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kutoa maji eneo la Segera hadi Kabuku mkoani Tanga kwa lengo la kukabiliana na adha ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo. Waziri Aweso amesema mradi huo unatarajia kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2025 ambapo tayari mkandarasi anaendelea na kazi.
Aidha Waziri Aweso ametoa wito kwa mkandarasi kuhakikisha anafanya kazi na kukamilisha kwa wakati pamoja na kuwashirikisha wananchi na viongozi wa eneo husika wakati wote wa ujenzi wa mradi huo. Aidha ameahidi kwamba Wizara ya Maji itahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa TAMISEMI Deogratius Ndejembi amesema tayari Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) imepokea shilingi bilioni 30 ambazo zitaanza kushughulikia changamoto mbalimbali za barabara hapa nchini. Ameongeza kwamba kwa upande wa Wilaya ya Handeni, Serikali tayari imetenga fedha kwaajili ya ujenzi wa barabara ya Sindeni – Kwedikazo ya kilometa 37.7 kwa kiwango cha lami. Amesema katika Wilaya hiyo TARURA itaanza mchakato mara moja wa kuhakikisha barabara zilizoharibiwa na mvua zinatengenezwa ili ziweze kupitika vema.