Mkuu wa kitengo cha uhusiano na elimu kwa umma tume ya maadili ya viongozi wa umma Halima Jumbe akitoa elimu ya tume hiyo kwa wananchi wa shehia ya Banko, Chimbuni na karakana.
Afisa kutoka tume ya maadili ya Viongozi wa umma Khamis Said Mohammed Akiwasilisha mada ya wajibu wa wananchi kwa tume hiyo huko skuli ya Chumbuni Wilaya ya Mjini
Afisa kutoka tume ya maadili ya viongozi umma wa Abdulatif Ali Ali akitoa elimu ya tume hiyo kwa wananchi huko skuli ya Chumbuni Wilaya ya Mjini
Mwananchi wa shehia ya chumbuni Ali Ali akichangia wakati wakipatiwa elimu juu ya tume ya maadili ya viongozi umma huko skuli ya chymbuni Mkoa wa mjini Magharibi.
PICHA NA FAUZIA MUSSA- MAELEZO ZANZIBAR
Na Fauzia Mussa, Maelezo.
Serikali imeunda Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kukuza uadilifu kwa Viongozi wa umma na kuimarisha uwazi, uwajibikaji, utii na usimamizi wa Sheria nchini.
Mkuu wa kitengo cha uhusiano na elimu kwa umma Halima Jumbe Said ameyasema hayo wakati akitoa elimu ya tume hiyo kwa wananchi huko skuli ya Chumbuni Wilaya ya Mjini.
Amesema miongoni mwa majukumu ya tume hiyo na kutoa elimu kwa jamii ili kuweza kuwajengea uelewa ikiwa ni pamoja na kupokea tuhuma za uvunjifu wa Maadili kutoka kwa Wananchi.
Alifahamisha kuna baadhi ya watu bado hawajakuwa na uelewa wa kutosha juu ya wajibu wao kwa Tume hiyo, hivyo wameamua kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wanachi ili kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
Akiwasilisha mada ya wajibu wa wananchi kwa Tume ya maadili wa Viongozi wa umma Afisa kutoka tume hiyo Khamis Said Mohammed amesema jamii inapaswa kutoa taarifa za uvunjwaji wa maadili kwa Tume hiyo ili Sheria ifate mkondo wake.
“Viongozi wa umma wanatoka na kuishi ndani ya jamii zetu jambo linalopelekea kuwafahamu vyema Viongozi hao na matendo yao tunachotaka ni kuona mnashirikiana na Tume hii kwa kuripoti taarifa zozote za kuvunjika kwa maadili na tume itamlinda na kumhifadhi mtu yoyote atakaetoa taarifa hizo ili kuona haki inapatikana kwa kila anaestahiki.” alisema Afisa huyo.
Aidha amewaomba Wananchi kuacha muhali na kuwatolea taarifa Viongozi wanaokwenda kinyume na maadili ili kuondosha athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza ikiwemo upotevu wa mali za umma na kuzorotesha maendeleo nchini.
Hata hivyo amesema ni jukumu la kila mtu kuchagua kiongozi bora na mwaminifu ili kuepuka kuwa na viongozi wasio na maadili ya kiutendaji na kuwataka wazazi kushirikiana kuwalea watoto katika maadili mema ili kutengeneza viongozi bora wa hapo baadae.
Kwaupande wake Afisa kutoka Tume ya maadili ya Viongozi umma wa Abdulatif Ali Ali amefahamisha kuwa miongoni mwa sifa zinazomtambulisha kiongozi asie na maadili ni pamoja na kutokujali mahitaji ya wananchi, kutumia vilevi kupindukia, kuaajiri kwa upendeleo, pamoja na kutumia mali ya umma kwa maslahi yake binafsi.
Asemesema upatikanaji wa utawala bora na maendeleo endelevu kuantokanana kuwa na viongozi wenye maadili mema hivyo amewaomba Wananchi kujitahidi kuwalea watoto katika maadili kwani kiongozi bora anatengenezwa ndani ya jamii.
“tujitahidi Watoto wetu waanze kufuata misingi ya maadili tangu nyumbani tukiwa na watoto,vijana,na viongozi wanaofuata maadili tutakua na maendeleo ya haraka sana nchini” alisema afisa huyo
Nao baadhi ya Wananchi waliopatiwa elimu hiyo akiwemo Ali Ali na Zainab Jaffar wamesema elimu hiyo imewasaidia kujua eneo husika la kupeleka kero za Viongozi wao ili kurahisha upatikanaji wa huduma za jamii.
Aidha wameiomba Tume hiyo kuanzisha mfumo maalum wa kuweza kufikisha malalamiko ya Viongozi wao ili kuepuka gharama za kufika Ofisi za Tume kuwasililisha malalamiko hayo.
Hata hivyo wameahidi kuwa Mabalozi wazuri kwa wenzao katika kufikisha elimu hiyo ili kuhakikisha haki zinapatikana.
Elimu ya kuitambua Tume ya Maadili ya Viongozi wa umma, imetolewa kwa Wakaazi wa Shehia tatu za Wadi ya Chumbuni ikiwemo Shehia ya Banko, Chimbuni na Karakana.