Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza kwenye mkutano na wanahabari ukumbi wa sekondari ya wasichana ya Dkt Samia Suluhu Hassan mjini Namtumbo,kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki
Na Albano Midelo,Namtumbo
WANAFUNZI walioripoti kidato cha kwanza katika shule za sekondari mkoani Ruvuma wamefikia asilimia 80.72 hadi kufikia Februari 16 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas katika mkutano na wanahabari uliofanyika kwenye ukumbi wa sekondari ya Dkt.Samia Suluhu Hassan mjini Namtumbo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa,idadi ya wanafunzi walioandikishwa elimu Awali hadi sasa imefikia asilimia 87.8 na wanafunzi wa darasa la kwanza imefikia asilimia 99 ambapo amesema hayo ni mafanikio makubwa katika Mkoa.
Hata hivyo amesema hivi karibuni umefanyika mkutano wa wadau wa elimu Mkoa wa Ruvuma ambao ulikuwa na lengo la kufanya tathmini ya hali ya elimu katika shule za msingi na sekondari.
“Tumekubaliana kila kiongozi lazima asimamie elimu ipasavyo,hii ni kuanzia viongozi walio katika ngazi ya Mkoa,Wilaya,Kata hadi ngazi ya Kijiji,kila kiongozi atapimwa utendaji wake kwa namna atakavyosimamia elimu’’,alisisitiza RC Thomas.
Akizungumzia kuhusu udumavu,Kanali Thomas amesema ili kukabiliana na udumavu,Mkoa unahamasisha upandaji miti ya matunda shuleni na kuhakikisha lishe bora inapatikana na kwamba Mkoa umeanzisha kampeni ya kupanda miche ya matunda tarehe 19 ya kila mwezi miti inapandwa katika shule za msingi na sekondari katika Mkoa mzima.
Katika kukabiliana na kero za wananchi,Mkuu wa Mkoa amesema ameunda Kamati ya Wataaalam kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi .
Amesema hadi sasa jumla ya wananchi wenye migogoro ya ardhi 106 wamewasilisha malalamiko yao ambapo wananchi 87 wamesikilizwa na kwamba hadi sasa jumla ya migogoro ya ardhi 42 imetatuliwa na kumalizika.
Ameongeza kuwa Mkoa pia umefanikiwa kutatua mgogoro wa wananchi wa vijiji vya Mkuka na Mkuani Kata ya Maguu wilayani Mbinga na wananchi wa Wilaya ya Nyasa ambapo mgogoro umetatuliwa kwa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kutoa eneo la ukubwa wa hekari 450 ambazo wananchi wa Mbinga wamepewa ili wawe na mradi wa panda miti kibiashara.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameweka kila tarehe 19 ya kila mwezi kukutana na wanahabari na kutoa taarifa mbalimbali za Mkoa ili wananchi waweze kupata taarifa zinazohusu Mkoa