Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi, Meja Jenerali Mstaafu Jacob Gideon Kingu (katikati-waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wapya wa Bodi hiyo baada ya kikao chao cha utambulisho na kupanga majukumu kilichofanyika hivi karibuni katika Ofisi Ndogo za Wakala wa Nishati Vijijini (REA) zilizopo jijini Dar es Salaam.
Na Veronica Simba – REA
Bodi ya Nishati Vijijini (REB) inayosimamia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imesema inategemea mafanikio makubwa katika kuiwezesha Wakala hiyo kutimiza azma yake ya kuwafikishia wananchi walioko vijijini nishati bora za umeme, mafuta na gesi.
Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Balozi, Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu baada ya kikao cha kwanza cha Bodi hiyo mpya kilicholenga kutambuana na kupanga majukumu.
“Kikao chetu kimeenda vizuri, tumechagua Kamati na kupangiana majukumu. Tunaamini na tunaahidi kuwa tutatekeleza majukumu yetu sawasawa na Sheria iliyoanzisha Wakala wa Nishati Vijijini inavyoelekeza,” amesema.
Aidha, Balozi Kingu amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi na amemshukuru Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ndiye Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko kwa kukamilisha mchakato wa uteuzi wa Wajumbe wa Bodi, jambo ambalo limeiwezesha kuwa Bodi kamili.
Akieleza zaidi kuhusu majukumu waliyojipangia, Balozi Kingu amesema mapema Mwezi Machi, Bodi itakutana katika kikao cha dharura kupitia na kujadili masuala mbalimbali ya Wakala ambayo yalikuwa yakisuburi baraka za Bodi ili kuyatolea maamuzi yatakayowezesha utekelezaji wake kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Katibu wa Bodi hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amepongeza Mamlaka za Uteuzi, kuteua watu makini, hodari na wachapakazi ambao amesema ni muhimu kuwa nao katika kuisimamia Wakala hiyo yenye majukumu makubwa yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
“REA ina jukumu kubwa ambalo linagusa maisha ya watu lakini pia linahusisha kiasi kikubwa sana cha fedha za Serikali. Kwahiyo, kuwa na Bodi nzuri iliyosheheni watu makini, kwetu sisi ni jambo la faraja,” amefafanua.
Mkurugenzi Mkuu, kwa niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi wote wa REA, ametoa ahadi ya ushirikiano kwa Bodi hiyo mpya ili kuhakikisha malengo ya Serikali kupitia majukumu yaliyokasimiwa kwa Wakala yanatekelezwa.
“Tunatamani kuona Watanzania wenzetu wanaoishi vijijini wanapata nishati bora kama ilivyo kwa wenzao wanaoishi mjini,” amesisitiza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wajumbe wa Bodi wamezishukuru Mamlaka za Uteuzi kwa kuwaamini na kuwapa jukumu hilo kubwa la kuisimamia REA ili kuendelea kuleta matokeo chanya.
Aidha, wamepongeza Bodi zilizotangulia kabla yao, Menejementi pamoja na Wafanyakazi wote kwa kazi nzuri waliyofanya tangu kuanzishwa kwa Wakala na kuahidi kuendeleza yote mazuri yaliyofanyika ili kuongeza tija.
Kikao hicho pia kilishirikisha Menejimenti ya Wakala ambapo Wakuu wa Idara na Vitengo waliwasilisha kwa Bodi taarifa za utekelezaji wa majukumu katika maeneo wanayosimamia kwa lengo la kuijengea Bodi uelewa na ufahamu kuhusu Taasisi hiyo waliyopewa jukumu la kuisimamia.
Januari 26 mwaka huu, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko aliwateua Florian Otman Haule, Lucas Charles Malunde, Mwantum Issa Sultan, Stephen Menard Mwakifamba, James Issack Mabula, Ahmed Martin Chinemba, Sophia Shaban Mgonja na Balozi Radhiya Naima Msuya kuwa Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, wakiungana na Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Gideon Kingu aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Septemba 2023 kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo.