Mkuu wa wilaya ya Lindi mkoani Lindi Shaibu Ndemanga,akizungumza katika kikao
cha tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa Maji unaotekelezwa na kanisa Anglikana Doyasis ya Masasi mkoani Mtwara katika kata za Mandwanga na Mnara Halmashauri ya wilaya Mtama,katikati Msaidizi wa Askofu wa Doyasisi hiyo Douglas Msigala na kulia Katitu Mtendaji Joyce Liundi.
Na Mwandishi wetu,
Mtama
SERIKALI wilayani Lindi,imeuagiza wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(RUWASA) wafungia mita za malipo ya kabla(Pre paid) wananchi waliounganishiwa huduma ya maji ili kuongeza mapato ya serikali.
Imesema,mita hizo zitasaidia kudhibiti upotevu wa maji, kuwa na uwazi kwenye makusanyo ya fedha za maji, kupunguza gharama za uendeshaji, kukomesha malalamiko ya kubambikiziwa Ankara za maji na zitawawezesha wananchi kupata huduma ya majimuda wote wa siku (saa 24).
Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa wilaya hiyo Shaibu Ndemanga,wakati akifunga kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa Maji baada ya ziara ya siku tatu ya kutembelea ujenzi wa miradi maji ya Mandwanga-Lindwandwali,Chiuta-Mikongi na Nyundo I-Nambahu inayotekelezwa na Kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi kwa kushirikiana na World Vision Tanzania.
Ameitaka RUWASA) kuzihamasisha taasisi za umma na binafsi kuunganisha maji kwenye taasisi zao ili ziweze kutoa huduma ya maji safi na salama kwa watu inaowahudumia.
Ndemanga,amewashukuru wadau Kanisa Anglikana Dayosisi ya Masasi kupitia mradi wa maji na usafi wa mazingira kwa kutenga zaidi ya Sh.bilioni 3.7 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji, miundombinu ya vyoo kwa shule za msingi, sekondari na zahanati; na utoaji wa elimu ya usafi na utunzaji wa mazingira, elimu ya kujitambua na uanzishaji wa vikundi kwa ajili ya kuongeza kipato cha familia.
Alisema,fedha zilizotolewa na kanisa Anglikana Dayosisi ya Masasi kutekeleza miradi ya maji katika kata ya Mnara na Mandwaga zingeweza kupelekwa katika wilaya na mikoa mingine hapa nchini.
Amewataka wataalam wilayani Lindi,kuwashirikisha wananchi pale wanapotaka kuanzisha miradi ya maendeleo na kuepuka kufanya shughuli zao kwa kificho ili kuepuka malalamiko ya wananchi.
Aidha,amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama) Mh. George Mbilinyi kuwatumia mafundi waliopatiwa mafunzo ya ujenzi wa vyoo bora kwenda kueneza elimu hiyo kwenye vijiji vingine vya Halmashauri hiyo.
Msaidizi wa Askofu wa Kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi Mchungaji Douglas Msigala alisema,Kanisa Anglikana litaendelea kushirikiana na wananchi pamoja na serikali katika kuboresha huduma za kijamii bila kujali itikadi za dini, rangi au kabila.
Hata hivyo,ameiomba serikali kushirikiana na kanisa hilo katika ulinzi wa miradi inayotekelezwa na kanisa hilo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na isaidie kuboresha maisha ya wananchi hasa wale wanaoishi maeneo ya vijijini.
“wananchi na watendaji wa serikali tunawaomba sana wawe waaminifu na waadilifu katika ujenzi na uendeshaji wa miradi inayotekelezwa na wadau wakiwemo sisi Kanisa Anglikana ili miradi hiyo ijengwe kwa viwango na kuleta tija kwa wananchi”alisema.
Katibu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Masasi Joyce Liundi alisema,mradi wa maji Mandwanga na Mnara katika Halmashauri ya Mtama unatekelezwa na Dayosisi hiyo chini ya usimamizi wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(RUWASA) na utahudumia zaidi ya wananchi 26,532 wa vijiji 10.
Alisema,mradi ulizinduliwa rasmi mwezi Juni 2023 na shughuli za utekelezaji ikiwemo ujenzi wa miundombinu zilianza mwezi Agosti baada ya kukamilika taratibu za manunuzi na unatekelezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 3,792,063,005.
Kwa upande wake Meneja mradi wa maji na usafi wa mazingira(WASH Project) Method Kamuhanda alisema, ujenzi wa miradi mitatu ya mwanzo inayohudumia vijiji sita (6) umefikia zaidi ya asilimia 85 na inatarajia kukamilika mwezi Machi mwaka huu.
Ametaja kazi zilizotekelezwa ni uchimbaji wa mitaro na kulaza bomba ambayo imefanyika kwa kushirikiana na wananchi,ujenzi wa matenki ya kuhifadhi maji, nyumba za mashine(Pump House) na kufunga umeme jua katika kijiji cha Mandwanga-Lindwandwali, Chiuta-Mikongi, na Nyundo I -Nambahu.
Pia alisema,katika utekelezaji wa mradi huo suala la usafi wa mazingira linapewa nafasi kubwa ambapo wametoa elimu na kuunda vikundi vya kuweka,kukopa na kuanzisha miradi ya kujiingizia kipato ili kukuza uchumi wa kaya na kutoa mafunzo ya mtazamo chanya na kuwajengea uwezo wa kutambua fursa zilizopo katika maeneo yao.
Diwani wa kata ya Mnara Athuman Mpole,ameipongeza Dayosisi ya Masasi kwa kazi nzuri ya kutekeleza miradi ya maji kwa kuishirikisha jamii na serikali,hata hivyo ameiomba Dayosisi kuharakisha utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maji kwenye vijiji vyake vya Chikombe na Mkanga II ambavyo hakuna huduma ya maji safi na salama.
Mtendaji wa kata ya Mandwanga Jenala Wanje alisema,kabla ya kujengwa kwa mradi wa maji Mandwanga-Lindwandwali wananchi walikuwa wanachota maji kwenye madimbwi na wengine kuchota maji barabarani ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu.
Wanje alieleza kuwa,mradi huo utakapokamilika kwa asilimia 100 utawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama na hivyo kupungua kwa baadhi ya magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyokuwa safi na salama.