Na John Walter-Babati
Serikali imesema itaendelea kushirikiana na Mashirika mbalimbali katika kuihudumia Jamii na kusaidia kwenye kutokomeza ukatili wa kijinsia na kuwa na ustawi wa jamii.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange wakati wa kikao na viongozi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, kilichofanyika Februari 16/2024.
Twange amesema kikao hicho kinafungua ukurasa rasmi wa muendelezo wa mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vilivyoshamiri katika wilaya ya Babati na mkoa wa Manyara na kwamba mbinu walizojadili zikifanyiwa kazi zitazaa matunda na kupunguza vitendo hivyo au kuvitokomeza kabisa.
Katika mapendekezo yao, wadau hao kutoka Ngo’s mbalimbali walieleza njia mojawapo itakayosaidia kuleta matokeo ni kuimarisha mabaraza ya watoto, kuimarisha Kamati za Ulinzi wa Wanawake na watoto za ngazi zote na kuhakikisha upatikanaji wa taarifa za matukio unaboreshwa.