Waziri wa Ardhi Nyumba, na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa akiongea na wananchi wa Ndachi Februari 15, 2024 Jijini Dodoma wakati akihitisha zoezi la Kliniki ya Ardhi ili kupisha uhakiki wa umiliki wa ardhi kwa wananchi wa kata ya Mnadani na Nkuhungu Jijini Dodoma. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo Bi. Rosemary Senyamule.
Na Eleuteri Mangi, WANMM
Waziri wa Ardhi Nyumba, na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amemwagiza Katibu Mkuu Wizara yake kuunda timu ya wataalam kutoka wilaya za mkoa wa Dodoma na mikoa jirani kufanya uhakiki wa umiliki wa ardhi kwa wananchi wa kata ya Mnadani na Nkuhungu Jijini Dodoma.
Waziri Silaa ametoa kauli hiyo Februari 15, 2024 Jijini Dodoma wakati akihitisha zoezi la Kliniki ya Ardhi ambayo imekuwa ikiendelea katika kata hiyo.
Kiongozi huyo ameagiza kuundwa kwa tume hiyo mara moja ikiwa ni hatua muhimu ya kutatua migogoro ambayo imedu mrefu ikichagizwa na baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ambayo tayari yamemilikishwa.
“Timu zitakuja uwandani kufanya uhakiki, tutafanya uhakiki shamba la kwanza mpaka shamba la 1397, tutafanya uhakiki wa mikataba iliyoingiwa kuangalia uhalali wake, iliingiwa kwa utaratibu gani, tutafanya uhakiki wa michoro ya mipango miji, tutafanya uhakiki wakina nani walikuwepo mwaka 2019, tutafanya uhakiki ni akina nani waliongezeka baada ya muda huo na nani amewaongeza, timu hizi zikimaliza kazi yake tutakutana tena hapa” amesema Waziri Silaa.
Waziri Silaa ametoa wito kwa watanzania kuwa suala la ardhi ni suala binafsi na kuwaomba watanzania wajiepushe na ufuatiliaji wa masuala ya ardhi kupitia vikundi vidogo vidogo na kutengeneza watu wanaojikusanya kwenye vikundi kuwatengenezea mazingira kwamba watasaidia kufuatilia jambo wanalofuatilia kuhusu ardhi na amewahimza kuwa Serikali ndiye msimamizi wa masuala ya ardhi na yanafuatiliwa kwa uadilifu na uaminifu wa hali ya juu.
Aidha, Waziri Silaa amewaonya viongozi wa kisiasa wa ngazi yeyote wa Chama cha Mapinduzi ama wa serikali kuwa ambaye atabainika kuchochea wananchi kukwamisha ama kutia hitilafu zoezi hilo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Zaidi ya hayo, Waziri Silaa amewataka wananchi kutoa ushirikiano wakati wote wa zoezi hilo na kuwaonya kutojichukulia sheria mkononi na kukwamisha zoezi la uhakiki wa ardhi na kusisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watu watakaokwamisha zoezi hilo.
Akimkaribisha Mhe. Waziri Silaa kuongea na wananchi wa Ndachi, Mkuu wa Mkoa huo Bi. Rosemary Senyamule amemshukuru Waziri kwa dhamira yake ya kumaliza kero ya ardhi kwa jiji la Dodoma na mkoa wa Dodoma kwa ujumla.