Taarifa kwa vyombo vya habari | 16 February 2024
Nusu ya waandishi wa habari nchini Tanzania wameripoti kutishwa au kunyanyaswa wakiwa kazini.
Tarehe 16 Februari 2024, Dar es Salaam: Nusu (50%) ya waandishi wa habari nchini Tanzania wameripoti kukumbana na vitisho, manyanyaso, mateso au kushambuliwa katika kazi zao. Wawili kati ya kumi (22%) wamekamatwa au kuzuiliwa na mamlaka, na idadi sawa na hiyo wamekumbana na unyanyasaji wa kijinsia (20%) au kunyang’anywa vifaa vyao vya kazi (20%).
Twaweza ikishirikiana na MISA-TAN, Jamii Forums, UTPC na TAMWA wametoa matokeo haya kwenye jarida la utafiti lenye kichwa cha habari Sautiza Waandishi: Uzoefu na maoni ya waandishi wa habari wa Tanzania. Jarida hili linawasilisha takwimu kuhusu uzoefu na maoni ya waandishi wa habari wa Tanzania. Maoni yalikusanywa kutoka kwa kwa wanahabari 1,202 wakiwemo waandishi wa habari, wahariri na wanablogu.
Wanahabari hawa wamepatikana kutokana na kanzidata za uanachama wa vyama mbalimbali vya vyombo vya habari ambavyo ni Chama cha Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Chama cha Wanawake Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA-Tan) na Jamii Forums.
Mahojiano yalifanyika kwa njia ya simu kati ya Septemba 23 na Novemba 7, 2023. Waandishi wengi wa habari wana ajira zisizo za kudumu, na zisizo za uhakika. Wawili kati ya kumi (20%) wanataja kuwa ajira zao ni za kudumu, ikilinganishwa na sita kati ya kumi (60%) wanaosema ni za muda na wawili kati ya kumi (18%) wanaosema wanaitwa kazini pale tu wanapohitajika.
Nusu (50%) wanayo mikataba iliyosainiwa. Waandishi wengi wa habari (63%) wanasema ni vigumu kujipatia kipato kinachokidhi mahitaji muhimu kupitia uandishi wa habari, wakati wachache (5%) wanasema si tatizo. Mmoja kati ya waandishi watatu (36%) wana kazi nyingine inayowalipa mbali na kazi yao ya uandishi.
Ni wanahabari wawili kati ya kumi (19%) tu ndio wangependelea watoto wao wafuate nyayo zao kuwa waandishi wa habari. Uzoefu wa waandishi wa habari kuhusu hatari wakiwa kazini ni mkubwa. Nusu (50%) wanaripoti kwamba wamewahi kutishiwa, kuteswa au kushambuliwa wakiwa kazini.
Waandishi wa habari kwa kiasi kikubwa wanawatuhumu maafisa wa serikali kama chanzo kikuu cha vitisho; zaidi ya nusu (56%) wanasema maafisa wa serikali ni chanzo kikuu cha vitisho, zaidi ya kundi lingine lolote. Wanahabari walio wengi (86%) wanasema rushwa ipo katika sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na 36% wanaosema rushwa ipo kwa kiwango kikubwa. Aina za rushwa zilizokithiri ni malipo kwa ajili ya kuchapisha (55%) au kutokuchapisha (53%) habari fulani.
Karibu wote (95%) wanasema wanakubali pesa kutoka kwa watu au taasisi zinazohusika na Habari, (23%) wanakubali mara kwa mara, na (72%) wameshakubali mara kadhaa. Mmoja kati ya kumi (10%) anaripoti kupokea ‘mara zote’ zawadi au pesa ili kubadilisha maudhui, na nusu (53%) wanasema wameshafanya hivyo angalau mara moja.
Aidha, waandishi wa habari wanahisi kwamba vyombo vya habari nchini Tanzania vina uhuru mdogo wa kufanya kazi bila kudhibitiwa au kuingiliwa. Wanahabari sita kati ya kumi hawajisikii huru kuripoti kuhusu rushwa (60%) au masuala yanayohusiana na vyombo vya ulinzi na usalama (61%).
Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, alisema: “Waandishi wa Habari wana majukumu muhimu sana nchini, yakiwemo kuwataarifu, kuwaelimisha na kuwaburudisha wananchi, pamoja na kuwawajibisha waliopo madarakani. Lakini mazingira wanayofanyia kazi si rafiki. Wanakutana na vitisho na unyanyasaji kwa sababu tu ya kusaka na kutangaza ukweli. Kipato cha walio wengi sio cha kutegemea, na hakikidhi mahitaji yao muhimu.
“Wanahabari wanayo haki ya kulindwa dhidi ya vitisho na unyanyasaji. Wanastahili kuwa na mikataba ya kazi na yenye maslahi mazuri. Sheria ziwalinde wanahabari, badala ya kuwatisha ili wasiibue ukweli. Nafasi ya waandishi wa habari katika jamii ni muhimu; sisi sote tunapaswa kufanya kila tuwezalo kuwalinda na kuwastawisha.”
—- Tamati —-
Kwa taarifa zaidi wasiliana na: Annastazia Rugaba | e: [email protected] | t: (+255) (0)687 222 197 Maelezo kwa Wahariri Jarida hili na takwimu zake zinapatikana: www.twaweza.org Twaweza inafanya kazi kupitia tafiti, ushahidi na kuchukua hatua ili kuonesha jinsi ambavyo wananchi wanaweza kushirikiana kutatua matatizo yao na kuifanya serikali iwajibike vizuri zaidi kwa wananchi; kuwezesha wananchi kupaza sauti zao kwenye masuala yanayohusu maslahi na uzoefu wao ili yasikilizwe na kuzingatiwa wakati wa kufanya maamuzi; na inahimiza kuweka mazingira wezeshi kwa ushirikishwaji wa wananchi na serikali kuitikia mahitaji ya wananchi nchini Tanzania, Kenya na Uganda. Tufuatilie kwenye Twaweza Tanzania (Facebook), @Twaweza_NiSisi (Twitter) na @Twaweza_EastAfrica (Instagram).
TAZAMA VIDEO HAPA