Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imefanya upasuaji wa kuweka mlango wa bandia kwenye moyo, hivyo kuwa Hospitali ya pili nchini kuanzisha huduma hiyo.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo BMH, Ahmed Toure, amesema leo upasuaji huo unafanyika pale milango wa kwenye moyo unapokuwa umeziba.
“Hivyo tumetoa mlango ulioziba ambao kitaalamu unaitwa valve na kuweka mlango wa bandia ili kuruhusu damu kuendelea kupita,” amesema Dkt Toure.
Upasuaji huu umefanyika kwenye kambi ya pamoja ya matibabu ya moyo kati ya madaktari wa BMH kwa kushirikiana na wenzao kutoka Uholonzi.
Dkt Toure amesema kuwa mlango huu unapobadilishwa mgonjwa anapona tatizo lililokuwa linamsumbua la mlango kuziba na damu itapita vizuri kama zamani.
“Mlango huu wa bandia ataishi nao maisha yake yote, na mzunguko wa damu unarudi kuwa wa kawaida,” anasema.
Kambi hii ya moyo ya wiki moja iliyoanza Jumatatu inatarajiwa kukamilika leo Ijumaa.