Kaimu Afisa habari na mawasiliano wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)mkoa wa Ruvuma Geddy Ndimbo kulia,akizungumza na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Masuguru wilayani Namtumbo kuhusu kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa maji ulioanza kutoa huduma katika kijiji hicho,katikati ni Mhandisi wa maji kutoka ofisi ya Ruwasa Namtumbo Salome Method.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Luhimbalilo wilayani Namtumbo, wakichota maji katika kituo cha kuchotea maji kilichojengwa kupitia mradi wa maji wa Luhimbalilo-Naikes mradi unaotarajia kukamili mwishoni mwa mwezi ujao.
Na Mwandishi Maalum,Namtumbo
CHANGAMOTO ya maji safi na salama kwa wakazi wa vijiji vya Luhimbalilo,Naikes na Luhangano wilaya ni Namtumbo mkoani Ruvuma inakwenda kumalizika na kuwa historia.
Hatua hiyo inatokana na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa), kuanza awamu ya pili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wa Luhimbalilo-Naikes utakaowanufaisha wakazi zaidi ya 15,542 wa vijiji hivyo.
Hayo yamesemwa jana na Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Namtumbo Mhandisi Salome Method,wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa na mkandarasi kampuni ya Trinitiy Manufacturing Service Ltd chini ya usimamizi wa Ruwasa wilaya ya Namtumbo.
Mhandisi Method alisema kuwa,mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili na umetengewa jumla ya Sh.bilioni 3,168,334,993.15 kati ya fedha hizo Sh.bilioni 1,710,024,283.15 zimetumika kutekeleza awamu ya kwanza katika kijiji Luhimbalilo.
Alisema,Sh.bilioni 1,458,310,710.00 zitatumika katika awamu ya pili ya mradi kwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ambayo ni kuboresha matenki mawili ya kuhifadhia maji, moja lenye ujazo wa lita 200,000 na lingine la ujazo wa lita 100,000.
Alitaja kazi nyingine zinazofanyika katika utekelezaji wa awamu hiyi ni uchimbaji wa mtaro na kulaza mabomba umbali wa kilomita 43,kujenga vituo 48 vya kuchotea maji katika vijiji vya Luhimbalilo,Luhangano na Naikesi na kujenga ofisi ya jumuiya ya watumia maji(CBWSO).
Kwa mujibu wa mhandisi Method,hadi sasa kazi zilizofanyika ni uchimbaji wa mitaro zaidi ya kilomita 21, na kulaza mabomba ya kusambaza maji umbali wa kilomita 19 na fedha zilizolipwa kwa mkandarasi wa awamu ya pili ikiwa ni malipo ya awali ni Sh.milioni 127,974,154.14.
Aidha alisema,Ruwasa wilaya ya Namtumbo imekamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Masuguru unaohudumia wakazi zaidi ya 3,264 kwa gharama ya Sh.milioni 315,483,914.00 kati ya Sh.milioni 402,000,000 zilizopangwa kutumika katika kazi hiyo.
Mkazi wa kijiji cha Luhimbalilo Said Juma,ameishukuru serikali kwa kujenga mradi huo kwani tangu kijiji hicho kilipoanzishwa miaka ya 70 hakijawahi kupata maji ya bomba.
Badala yake,walikuwa wanatumia maji ya visima na mito ambayo hayakuwa safi na salama na hivyo kusababisha magonjwa ya matumbo ikiwemo kipindu pindu mara kwa mara.