Mwakilishi wa Mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha ,Dk Leticia Rwabishugi akifungua mafunzo hayo chuoni hapo
Mratibu wa jinsia na maendeleo ya mtoto kutoka halmashauri ya jiji la Arusha ,Habiba Madebe akizungumza katika mafunzo hayo .
Viongozi wa wanafunzi, wawakilishi wa madarasa na watoa huduma wasio wafanyakazi wakifuatilia mafunzo hayo chuoni hapo.
Happy Lazaro,Arusha
Arusha .Chuo cha uhasibu Arusha (IAA) kimetoa mafunzo maalumu ya kujenga ufahamu kuhusu ukatili wa kijinsia kwa Wafanyakazi wa chuo ,Viongozi wa wanafunzi pamoja na wawakilishi wa madarasa na watoa huduma wasio wafanyakazi huku wakitakiwa kulitumia dawati kwa kuripoti matukio ya ukatili na kuweza kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mwakilishi wa Mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha ,Dk Leticia Rwabishugi amesema kuwa mafunzo hayo yametolewa kwa lengo la kukumbushana wajibu mbalimbali katika swala zima la ukatili wa kijinsia hapo chuoni.
“Hapa chuoni tuna dawati linaloshughulikia maswala hayo ila leo tumeweza kukumbushwa wajibu wetu sambamba na kuwataka kulitumia ipasavyo dawati hilo ambalo lipo hapa chuoni na linaendelea kushughulikia maswala mbalimbali ya ukatili chuoni hapa.”amesema .
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kufanya wafanyakazi pamoja na watoa huduma wajue dawati lipo na wasikubali kunyanyasika na kuweza kuripoti matukio hayo sehemu husika endapo yatajitokeza.
Dk.Rwabishugi amewataka viongozi wa wanafunzi na wawakilishi wa madarasa kutokubali kunyanyaswa bali wahakikishe wanalitumia dawati hilo katika kuripoti matukio endapo yakijitokeza na kuweza kuchukuliwa hatua haraka kwani hilo ndilo lengo kuu la kuwepo kwa dawati hilo chuoni hapo.
Mafunzo haya ni utekelezaji wa majukumu ya Dawati la Jinsia ; Kauli Mbiu yetu ni “Usikubali Kunyanyasika, Dawati lipo”,hii itawasaidia kujua kwamba wanapokutana na changamoto za kijinsia watoe taarifa na watasaidiwa” amesema Dk Rwabishugi.
Kwa upande wake, Mratibu wa dawati la jinsia chuoni hapo ,Dk Theophil Assey amesema kuwa ,mafunzo hayo yamelenga kutoa elimu kwa jamii hiyo ya chuo cha uhasibu Arusha ili waweze kuwa mabalozi katika nafasi zao na hatimaye kuweza kukemea vitendo hivyo na kuripoti sehemu husika kwa wakati.
Amesema tangu dawati hilo limeanzishwa limetoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jumuiya ya IAA na kuanzisha klabu za wanafunzi za kupinga ukatili wa kijinsia; ikiwa ni njia ya kuongeza uelewa juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia kwa makundi hayo.
“Nia yetu kama dawati si kusubiri tatizo la ukatili wa kijinsia litokee halafu tulishughulikie, sisi tunatoa elimu ili kuzuia maana tunafahamu kuzuia ni bora kuliko kushughulikia madhara”, amesema Dk. Assey.
Naye Mratibu wa jinsia na maendeleo ya mtoto halmashauri ya jiji la Arusha ,Habiba Madebe amesema kuwa,kupitia mafunzo hayo wameweza kutoa elimu na kujifunza aina za ukatili na namna ya kukabiliana na ukatili huo ili kwa pamoja wanafunzi hao waweze kushirikiana na kuwa mabalozi wa kupinga vitendo hivyo chuoni hapo.
Habiba amesema kuwa,kupitia mafunzo hayo wameweza kupata uelewa mpana zaidi kuhusiana na maswala hayo ,na matarajio ni kuona matukio hayo yanapungua kabisa kupitia elimu iliyotolewa.
Kwa upande wake ,Makamu wa Rais serikali ya wanafunzi ,Tedy Mbaga amesema kuwa,wao wapo kwa ajili ya kusimamia wanafunzi chuoni hapo na uwepo wa mafunzo hayo ni muhimu sana kwani wanakumbushwa wajibu wao sambamba na kuwaunganisha wanafunzi ili wakikutana na changamoto yoyote waweze kuripoti kwenye dawati hilo.
“Sisi kama viongozi tutakuwa tayari kuripoti sehemu husika matukio yoyote ya ukatili endapo yatajitokeza chuoni hapa kwani uongozi wa chuo umejidhatiti kuondoa maswala ya unyanyasaji vyuoni na kamwe hawatanyamaza “amesema .